HabariLifestyleNews

Seneta Miraj ahimiza Ushirikiano Kuinua Viwango vya Elimu Mombasa

Seneta maalum kaunti ya Mombasa Miraj Abdillah amekariri haja ya wadau mbalimbali katika sekta ya elimu kushirikiana ili kuimarisha viwango vya elimu miongoni mwa wanafunzi.

Akizungumza leo hii wakati ulimwengu unapoadhimisha siku ya elimu duniani, Miraj ameeleza haja ya kurudisha hadhi ya elimu kama ilivyo kuwa awali katika kaunti hiyo.

“ Sisi viongozi, nyinyi wazazi na watoto kama wahusika wakuu katika masuala ya elimu tuweze kuweka vichwa vyetu chini kwa sababu mji wa mombasa umetambulika kwa ajili na kwa sababu ya wasomi wengi ambao wamechipuka wakati wa nyuma.

Shule kama Aldina Visram, Mama Ngina, Shimo la Tewa zilikuwa zikiwika sio katika michezo tu ya shule lakini pia katika masomo walivyokuwa wametaradai.” Alisema Bi Miraj.

Miraj alisema kupitia mswada aliouwasilisha katika bunge, kila mtoto hasa watoto wa kike waliopata ujauzito wanapata fursa kufufua ndoto zao kwa kufadhiliwa ili kuendelea na masomo.

Aliongeza kuwa kupitia Wakfu wake wa Mama Haki, uongozi wake seneta huyo utahakikisha kuwa hakuna mtoto yeyote atakayesalia nyumbani na kukosa kufika shuleni kupitia kampeini yake na ushirkiano wa wadau mbalimbali.

“Sisi kama Mama Haki Foundation tutahakikisha hakuna mtoto wa kike atakosa kuingia shule,”  alisisitiza.

Vile vile Miraj maarufu Mama Haki aliwahimiza wazazi na wanafunzi waliopata alama 350 katika mtihani wa kitaifa wa KCPE kutuma maombi ya ufadhili chini ya mradi wa ‘Mtoto asome initiative’.

Kulingana na Miraj, mradi huo ulizinduliwa mwaka jana 2023 ambapo takriban wanafunzi 40 walifadhiliwa kupitia kwa mpango huo.

“ Siku hii ya leo ningependa kuwatunukia jamii yangu ya mombasa na kuwajulisha ya kwamba katika mradi wa mtoto asome initiative ambao unasimamiwa na Wakfu wa Mama Haki, jana tuliweza kuzindua rasmi link ambayo wale watoto ambao wamepata alama ya 350 na hawajui watajiunga vipi na kidato cha kwanza wanaweza kujaza link hiyo ili na wao waweze kua miongoni mwa wale watakaopata ufadhili kutoka kwa wakfu wa Mama Haki,” alihimiza Bi Miraj.

Unaweza kupakua fomu hiyo kupitia https://docs.google.com/forms/d/e/1FAIpQLSfY4SHhK_ynJot-7vYmrSHbvS2YoDl6Du35gDV-yRaCB_cIkA/viewform?pli=1

Haya yanajiri siku moja tu baada ya msemaji wa mradi huo wa ‘Mtoto asome initiative’ Abdallah Gatana kusema kuwa takribani asilimia 40 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa KCPE kote nchini wamesalia majumbani kutokana na hali ngumu ya Maisha.

BY MJOMBA RASHID