Jumla ya washukiwa 39 wa mauaji ya halaiki ya watu katika msitu wa Shakahola wamekana mashataka yote 17 dhidhi yao mbele ya Hakimu Nelly Chipchirchir katika mahakama ya watoto ya Tononoka hapa mjini Mombasa.
Wakiongozwa na mhubiri tata Paul Mackenzie washukiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kuwatesa watoto kinyama, kusababisha vifo vya watoto kinyume cha sheria,kuwanyima haki yao ya elimu na chakula miongoni mwa mashtaka mengine.
Mawakili wa washukiwa hao wakiongozwa na Wycliffe Makasembo waliiomba mahakama kupewa stakabadhi za zenye ripoti ya ushahidi wa madai dhidi ya wateja wao ili wazihakiki na kuzitathmini, ombi ambalo mahakama ya watoto ya Tononoka ilikubaliana nalo.
Akitoa mwelekeo zaidi wa kesi hiyo, Hakimu mkuu wa mahakama hiyo Chipchirchir alisema mahakama hiyo ilibaini kuwa washukiwa wote waliyapinga madai dhidi yao.
“ shtaka la 12 mshtakiwa wa kwanza hadi thelathini na moja amekataa hayo mashtaka, shtaka la 13 mshtakiwa wa kwanza hadi thelathini na moja na mshtakiwa wa 37 amekataa hayo mashtaka, shtaka la 14 mshtakiwa wa kwanza na mshtakiwa wa 37 wamekataa hayo mashtaka, shtaka la 15 mshtakiwa wa kwanza hadi thelathini na mbili mumekataa hayo mashtaka vile vile shtaka la 16 mshtakiwa wa kwanza na mshtakiwa wa 32 mumekataa hayo mashtaka, shtaka la mwisho na la 17 mshtakiwa wa kwanza hadi mshtakiwa wa 17 koti imenakili kwamba mumekataa hayo mashtaka”
Mashtaka ya leo dhidi ya washukiwa hao ni ya tatu chini ya wiki mbili baada ya baadhi yao kushtakiwa tena katika mahakama ya shanzu kwa tuhuma za ugaidi katika Mahakama ya Mombasa kwa madai ya mauaji. Januari 25 wakishtakiwa kwa kosa la kudhulumu kinyama watoto msituni Shakahola.
Ikumbukwe kuwa 39 hao ni miongoni mwa washtakiwa 95 walioshatakiwa katika mahakama ya Mombasa mnamo Jumatatu wiki hii kwa makosa 238 ya mauaji ambayo waliyakana mbele ya Hakimu Mkuu Alex Ithuku.
Kesi dhidi ya washukiwa hao za madai ya mauaji na dhuluma dhidi ya watoto msituni Shakahola zitatajwa mahakamani Februari tarehe 13 na 15 mwaka huu katika mahamaka ya Mombasa na Tononoka mtawalia.