HabariNews

Samaki wa Ziwa Nakuru Hawafai Kuliwa na Binadamu, Asema Mvurya

Samaki wanaovuliwa kutoka Ziwa Nakuru hawafai kwa matumizi ya binadamu, hili ni Onyo la Waziri wa Madini, Uchumi samawati na Masuala ya Baharini Salim Mvurya

Akizungumza katika Kaunti ya Embu siku ya Jumatano 24 Januari baada ya kufanya mazungumzo na Gavana Cecile Mbarire, Mvurya alisisitiza kwamba majaribio ya hivi majuzi yaliyofanywa yalibaini kuwa samaki wanaopatikana kutoka Ziwa Nakuru walionyesha kuwa na kiwango cha juu cha arsenic, kemikali inayopatikana katika madini mengi Ulimwenguni.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), matumizi ya muda mrefu ya kemikali ya arseniki kupitia unywaji wa maji na vyakula unaweza kusababisha saratani na vidonda vya ngozi.

Zaidi ya hayo, kemikali hii ilihusishwa na ugonjwa wa moyo na mishipa pamoja na ugonjwa wa kisukari. Dalili za moja kwa moja za sumu ya arseniki ni pamoja na kichefuchefu, kutapika na kuhara.

Katika Baraza la Mawaziri lililopita tuliloketi Sagana, nilitoa mada kuthibitisha kwamba samaki wa Ziwa Nakuru hawafai kuliwa na binadamu. Tuna samaki ambao wameonyesha kiwango cha asilimia 32 ya madini ya arseniki ambayo si mazuri kwa matumizi ya binadamu. ,” alisema Waziri Mvurya.

Kwa hiyo ni kweli tulithibitisha kuwa haifai kwa matumizi ya binadamu na kwa hiyo tumeunda timu ya mashirika mengi. Idara za uvuvi na uchumi wa bluu, mazingira na wengine wanaangalia suala hili.”

 

Mvurya hata hivyo alifichua kuwa mazungumzo yake na Gavana Mbarire yamezaa juhudi zinazolenga kuchochea shughuli za uchimbaji madini katika Kaunti ya Embu, akisisitiza kwamba uchimbaji madini utaleta manufaa ya pamoja kwa kaunti hiyo, wakazi wake na serikali ya kitaifa kwa ujumla.

Tayari tumekubaliana na serikali ya kaunti na maafisa wa serikali ya kitaifa walioko hapa kwamba kwa kuendelea, tutashirikiana haswa katika suala la uchimbaji haramu ambao umekithiri nchini,” alisema.

Pia tumejadili eneo zima la utoaji leseni kwa sababu tulifungua usitishaji huo Oktoba mwaka jana na sasa tunapokea maombi ya wawekezaji wa madini. Pia tuliangalia suala la manufaa kwa serikali za kaunti na kitaifa na jamii ya eneo hilo.

BY NEWS DESK