HabariNews

Kijana auawa kwa madai ya nguvu za mapepo Malindi

Maafisa wa usalama eneo la Malindi kaunti ya Kilifi wanasema wanachunguza kisa ambapo kundi la vijana lilimvamia na kumuuwa kijana wa umri wa makamo siku ya jumapili mchana tarehe 28 januari mwaka huu katika Kijiji Cha Sabaki viungani mwa mji wa Malindi.

Akithibitisha kisa hicho kamanda wa polisi eneo hilo Wilmot Mwakio alisema maafisa wake tayari walianzisha msako mkali kuwatafuta vijana wote waliohusika katika kisa hicho.

Mwakio alidokeza kuwa Mwalimu Charo, mwenye umri wa makamo alikumbana na mauti yake mikononi mwa vijana anaowafahamu vyema kutokana na madai ya kuwa na nguvu za mapepo.

Kamanda huyo vile vile aliwaonya vijana dhidi ya kuchukua hatua mikononi kutokana na madai wasiyoweza kuyadhibitisha huku akionya huenda wakachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha kulingana na wenyeji maafisa wa usalama walifika kuchelewa eneo la tukio hivyo kutoa mwanya wa vijana hao kutekeleza mauwaji hayo.

Kwa sasa mwili wa mwendazake umehifadhiwa katika chumba Cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya Malindi ukisubiri kufanyiwa upasuaji.

BY JOSEPH YERI