Mmiliki wa kituo haramu cha Kujaza gesi kilicholipuka wiki jana huko eneo la Embakasi na kuwaua takribani watu 6 hatimaye amejisalimisha kwa maafisa wa polisi.
Inaarifiwa kuwa jamaa huyo anayemiliki mtambo alihojiwa na maafisa wa DCI kuhusu mtambo huo ambao ulipelekea maafa hayo na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa.
Maafisa wamekuwa wakiwasaka washukiwa saba kuhusiana na mlipuko akiwemo Derrick Kimathi mmiliki wa mtambo haramu wa kujaza gesi, Steve Kioko mshirika wake Kimathi, dereva wa lori aliyeshukiwa kusababisha mlipuko huo ambaye bado hawajathibitisha kama alitoroka au alikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa; na maafisa wanne wa NEMA ambao walisimamishwa kazi kwa madai ya kutoa leseni kinyume cha sheria kwa kampuni ya Kimathi.
Kupitia wakili wake Kimathi aliwaambia maafisa kuwa yupo katika biashara ya usafirishaji wa LPG na kuwa mwaka uliopita alituma maombi kwa Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Mafuta (EPRA) kupata leseni ili kuendesha mtambo wa kujaza gesi katika eneo hilo lakini maombi yalikataliwa.
Hata hivyo amekana ripoti na madai kuwa eneo ambalo mkasa ulitokea kulikuwa na mtambo haramu wa kujaza gesi akieleza kuwa eneo hilo kwa miaka limekuwa ni gereji.
BY NEWSDESK