HabariLifestyleNews

Hatma ya Masomo kwa Maelfu ya Wanafunzi Tana River i njia Panda

Huenda maelfu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa KCPE mwaka 2023 katika kaunti ya Tana River wakashindwa kuendelea na masomo yao ya shule ya upili.

Gavana wa kaunti hiyo meja mstaafu Dhadho Godhana amesema idadi hiyo huenda ikasalia majumbani kutokana na umasikini uliokithiri.

Akizungumza eneo la Mikinduni kaunti hiyo ya Tana River, Gavana Godhana amesema zaidi ya watahiniwa 6,000 huenda wakaacha masomo kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

Amesema hali hiyo imechangiwa na mafuriko yaliyoshuhudiwa miezi iliyopita na kwamba kungali na hofu kuwepo kwa ongezeko la idadi ya wanafunzi kuacha masomo.

“Tulipata wanafunzi 3,044 vijana wa kuenda Form 1 na tumekuwa na 3,129 wasichana pia na kati ya hao, 898 hawajaenda shule na kati ya hao wameenda karibu asilimia 40 hadi 50 wameenda kushika tu nafasi na asilimia 20 yao mwezi huu wa Februari watafukuzwa kurudi nyumbani kwa sababu ya karo,” alisema.

Gavana huyo hata hivyo ameahidi kuidhinisha mpango wa Hazina ya ufadhili wa masomo, mpango ambao utajadiliwa na kamati ya elimu kati bunge la kaunti hiyo ili kusaidia wanafunzi kutimiza malengo na ndoto zao za kimasomo.

“Kama viongozi tunahitajika kushughulikia sana matatizo haya na tuyafutia njia kuyamaliza. Mimi sitachoka kusema lile ni sahihi na kufuata, nitaika Mwenyekiti wa kamati ya elimu bungeni ili kujadili mpango wa Hazina kuhusu ufadhili wa masomo kwa wanafunzi.” Alisema.

BY NEWSDESK