HabariNewsSiasa

Wakulima kaunti ya Kilifi waepushwa dhidi ya mbegu ghushi.

Wakulima wakiendelea kutayarisha mashamba yao msimu wa upanzi unapokaribia, serikali ya kaunti ya Kilifi imesema imeweka mikakati ya kukabiliana na usambazaji wa mbegu ghushi ili kuwaepushia hasara wakulima.

Baadhi ya mikakati iliyowekwa na serikali hiyo ni kuruhusu uuzaji wa mbegu zilizopasishwa na vitengo husika pekee nchini, kama vile Kebs, Kephis, Karlo miongoni mwa vitengo vingine ili kuwaepushia wakulima hasara ya kukosa mavuno.

Kwa mujibu wa katibu wa idara ya Kilimo kaunti ya Kilifi Teddy Yawa, hatua hiyo itachangia kupatikana kwa chakula cha kutosheleza mahitaji ya wakazi maarufu “usalama wa chakula” na kuiondoa kaunti ya Kilifi kwenye orodha ya kaunti zinazoathiriwa zaidi na baa la njaa nchini.

“Huwa tunazingatia kwanza, kila mbegu ambayo inaletwa lazima iwe na chapa cha Kenya Plant Health Inspectorate Services KEPHIS, unajua hawa ndio huangalia usawa wa mbegu, hutoa sanitary certificate, ya pili hapa kwetu tuna KARLO, mara nyingi sisi huwategemea wao.

“Mbegu watakayoisema inafaa basi sisi tunanunua, halafu pia kuna shirika ambalo linahusika na kuthibitisha ubora wa bidhaa KEBS, mali yoyote ambayo haina chapa cha KEBS hiyo ni mali ambayo haijapewa uwezo wa kutumika na wananchi.

“Kwa hivyo huwa tunaangalia sana haya maneno mawili hasa kitu kama mbegu, lazima iwe imepigwa muhuri wa KEPHIS.” Alisema Yawa.

Aliongeza kuwa wauzaji walioidhinishwa pekee ndio watakaoruhusiwa kuuza mbegu huku akitoa onyo kuwa yeyote atayepatikana akiuza mbegu ambazo hazijapasishwa atachukuliwa hatua za sheria.

“Mbegu zetu lazima zinunuliwe kutoka kwa msambazaji aliyethibitishwa mfano Kenya Seed ni msambazaji aliyethibitishwa, Bayer and Bayer, Sinjeta na kampuni kama hizo ni baadhi ya zile zilizothibitishwa.

“Kwa hivyo wakati unapotuletea mbegu ambazo hatujui zimepatikana wapi na wakati inakibandiko cha kampuni zilizothibitishwa na hizo mbegu ni mbaya basi hatutakuwa na budi ila kukushtaki mahakamani.

“Kwa hivyo ole wao wale wanaopelekewa mbegu ambazo hazina vibandiko vya wasambazaji waliothibitishwa.” alisema Yawa.

By Erickson Kadzeha.