Akizungumza katika Kongamano la Baraza la Leba la ARLAC linaloendelea hapa mjini Mombasa, Waziri Bore amesema tayari wizara yake imefanya mazungumzo na wizara wa leba Ujerumani na kilichosalia ni maafikiano tu ya mwisho kabla ya pande zote mbili kutia saini rasmi muktaba wa maelewano
Kwa mujibu wa waziri huyo, vijana wasio na ajira nchini wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kutafuta ajira katika mataifa ya ughaibuni ambako kulingana naye, kuna nafasi tele za kazi ambazo ni nadra kupatikana humu nchini.
Waziri Bora ameongeza kuwa serikali kuu kupitia wizara yake ya leba zimo mbioni kutafuta nafasi zaidi za kazi mataifa ya kigeni akiongeza kuwa wataendelea kushirikiana na wizara ya masuala ya Kigeni kuona haki za kikazi za wakenya walioko ughaibuni zimelindwa.
“Ningependa kugusia kwamba nilikuwa kule Ujerumani ambapo nilienda kuwatafutia wakenya kazi.Nilikutana na waziri wa leba wa Ujereumani, pamoja tukaanzisha mchakato wa muktaba ya maafikiano ya kazi ili kwamba wakenya ambao wataenda kule,wapate kazi nzuri na walipwe vizuri…”
“…walituambia kuwa wana nafasi na ajira mia mbili hamsini ambazo zinapatikana.Asilimia kubwa ya watu wasio na ajira ni vijana, ninawashauri vijana waende uko.”Alisema Florence Bore.
Na huku Kongamano la ARLAC likilenga kubuni nafasi za ajira miongoni mwa vijana wa wanachama ,waziri Bore amesema serikali ya Kenya itashirikiana kikamilifu kufanikisha azima ya baraza hilo la leba.
Kwa mujibu wa waziri huyo, azima hiyo itafikiwa iwapo hamasisho la matumizi ya Rasilimali na malighafi yaliyopo litatolewa kikamilifu na mafunzo ya umilisi katika vyuo vya Kiufundi na vile vya anuai kutolewa ili kuwapa wafanyakazi stadi za kikazi zitakazowasaidia katika soko pana la kimataifa lililo na ajira endelevu.
“Kenya imejitolea kuwa mojawapo ya mataifa yatakayoleta mustakabali wa ufasi ndani ya muungano wa Leba wa ARLAC. Kama taifa, tutaunga mkono maendeleo endelevu yanayonuia kupunguza gharama ya maisha, kubuni nafasi za ajira, kuafikia usawa wa kimaendeleo, kuongeza mapato ya kigeni, utoaji wa mafunzo ya teknohama na utoaji wa mafunzo ya umili.” Alisema
Kauli ya waziri huyo kuhusu nafasi za ajira katika mataifa ya ughaibuni inaoana na ya Rais William Ruto hapo jana kaunti ya Kiambu, ambapo alisema serikali yake kufikia sasa imewatafutia ajira vijana zaidi ya milioni moja katika mataifa ya Kigeni.
By ISAIAH MUTHENGI