Wakenya wamemiminika katika mitandao mbalimbali ya kijamii kueleza hisia mseto kufuatia kupotea kwa nguvu za umeme mara kadhaa rais William Ruto alipokuwa akihutubia mawaziri.
Baadhi ya Wakenya sasa wamemtaka rais kumsimamisha kazi mara moja Waziri wa Kawi Davis Chirchir kwa kile wanachokihisi kuwa utepetevu na kuzembea kazini.
Hata hivyo wengine wametaja kama mazoea kwa kinachowafika kila uchao wakisema rais anapaswa kupitia kile wanachopitia wakenya.
Mnamo siku ya Jumatano, Rais William Ruto alilazimika kuhutubu gizani huko Naivasha wakati wa kilele cha mkutano wa baraza la mawaziri na Serikali Kuu baada ya umeme kupotea mara kadhaa.
Katika video iliyonaswa na NTV kwenye mkutano huo rais Ruto alisikika akiongea kutoka gizani huku akiuliza kipi kilikuwa kikiendelea kabla ya umeme kurudi tena dakika chache baadaye.
Taa zilizimika mara kadhaa kwa angalau sekunde tano huku Mkuu wan chi akijaribu kuzungumza kupitia kipaza sauti kwa muda kabla taa kuwashwa tena.
“Nini kinaendelea? Tupo…oh, sawa,” Alisikika Ruto huku akijaribu kipaza sauti.
Lakini kama hiyo haikuwa aibu tosha kutoka kwa Kampuni ya Umeme, KPLC, rais tena alilazimika kumaliza hotuba yake gizani baada ya umeme kupotea tena alipokuwa akikaribia kukamilisha hotuba.
Itakumbukwa kuwa katika siku za hivi karibuni Kenya Power imekuwa ikikumbwa na hitiliafu na kuyumba kwa mitambo yake ya kuzalisha umeme na kulitumbukiza taifa gizani kwa saa kadhaa.
BY MJOMBA RASHID