Baadhi ya Viongozi wa Kisiasa wanaoegemea mrengo wa Serikali, Kenya Kwanza, sasa wanasema rais William Ruto hatakuwa na mpinzani wa haja na atachaguliwa tena bila kupingwa katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Magavana na Wabunge wa Kenya Kwanza wamesema hatua za kisiasa za hivi karibuni zilizochukuliwa rais Ruto zimeashiria mkakati mwafaka wa kupenya hata katika ngome kuu za upinzani huku akijitengenezea nafasi ya kuchaguliwa tena.
Caleb Mule ambaye ni Mbunge wa Machakos anasema kuwa kujitolea kwa rais Ruto kuunga mkono azma ya Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa Muungano wa Afrika AU, ni sehemu ya mpango kupata uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wa Odinga na hivyo kuimarisha azma yake ya kuchaguliwa tena mwaka 2027.
Kwa upande wake Mbunge wa Emurrua Dikirr, Johanna Ng’eno amebaini kuwa Ruto ana mpango wa kupunguza upinzani wa kisiasa nchini ilia pate kuweka mazingira mwafaka ya kuleta maendeleo.
Ni kauli iliyoungwa mkono na Mbunge wa Manyatta Mukunji Gitonga na mwakilishi wa Wanawake wa Laikipia Jane Kagiri.
Huku hayo yakijiri, Gavana wa Uasin Gishu Jonathana Bii alimsifia Odinga kwa kumtaja kuwa kiongozi bora katika nafasi hiyo akisema kuwa ana ufahamu bora katika ulingo wa kisiasa, sio tu nchini bali katika bara la Afrika.
Kadhalika Bii alisema kuwa uamuzi huo utapisha nafasi kwa rais William Ruto kuomba kura mwaka wa 2027 katika ngome za ODM bila tashwishi yoyote.
BY MJOMBA RASHID