HabariLifestyleMombasaNews

Mashirika ya Kijamii Pwani Yashinikiza Bunge la Seneti Kutopitisha Mswada wa Nyumba za Bei Nafuu

Muungano wa Mashirika ya kutetea haki za kibinadam Ukanda wa Pwani, Coast civil society network, umelitaka Bunge la Seneti kutupilia mbali Mswada wa ujenzi wa nyumba za gharama ya bei nafuu Mwaka 2023 kwa kile wanachokitaja kuwa umekiuka sheria.

Mwenyekiti wa Muungano huo Zedekiah Adika amesema kuwa mswada huo unakiuka katiba kwani serikali za kaunti ndizo zenye majukumu ya kufanikisha mradi huo wala sio serikali kuu.

Amesema mswada huo utakaotoa fursa kwa serikali ya Kitaifa ambayo tayari inaendeleza mpango huo kuzidi Kwenda kinyume cha katiba ya taifa hasa ikizingatiwa kuwa serikali kuu inapaswa kutoa sera na mwongozo na si kuchukua jukumu la ujenzi wa nyumba hizo.

“Jingine ambalo muungano huo unahofia huenda likafanyika iwapo seneti itaupitisha mswada huo ni kuhamishwa kwa umiliki wa ardhi za umma ambazo ujenzi huo utaendelezwa hadi kwa watu binafsi, na hivyo basi kushinikiza bunge la Seneti kusimama imara kulinda ugatuzi na kutoruhusu kupitishwa kwa mswada huo.

Aidha mashirika hayo yameonyesha kughadhabishwa na hatua ya viongozi wabunge kutoka ukanda wa pwani kupitisha mswada huo licha ya kuwa na dosari.

Haya yanajiri wakati ambapo tayari Bunge la Kitaifa liliupitishwa mswada huo baada ya wabunge 141 kupiga kura ya kuunga mkono dhidi ya wabunge 58 walioupinga mswada huo.

BY DAVID OTIENO