HabariNews

Pigo kwa Kaunti; Serikali Kuu Yawatengea Mgao mdogo zaidi wa Fedha Walizohitaji mwaka wa Kifedha 2023/2025

Serikali za kaunti zimepata pigo baada ya kutengewa Sh391 bilioni na serikali kuu katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025 badala ya mgao wa Sh450 bilioni ambazo magavana waliitisha.

Kwa upande mwingine, serikali ya Kitaifa imetengewa shilingi trilioni 2.5 za mapato ya serikali katika mwaka huo wa kifedha unaoanza Julai 1, 2024.

Aidha, kulingana na Mswada wa Ugavi wa Mapato wa 2024 uliowasilishwa katika Bunge la Kitaifa na mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Ndindi Nyoro mnamo siku ya Jumatano, Hazina ya Usawazishaji Kimaendeleo NG-CDF imetengewa Sh7.8 bilioni.

Baraza la Magavana (CoG) limekuwa likishikilia kuwa serikali 47 za kaunti zitengewe Sh450 kama mgao wa kifedha kutoka kwa bajeti ya Sh470 bilioni lililopendekeza awali.

Aidha, Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) ilikuwa imependekeza kuwa serikali za kaunti zitengewe Shilingi bilioni 407 badala ya Sh416 bilioni.

Kupunguzwa kwa mgao huo kunajiri licha ya wiki jana, mwenyekiti wa CoG Anne Waiguru aliyefika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na kulalamikia mwenendo wa serikali kuendelea kukwamilia fedha zinazofaa kuelekezwa kwa serikali za kaunti.

Bi Waiguru ambaye ni Gavana wa Kirinyaga alilalamika kuwa baadhi ya serikali za kaunti hazijalipa mishahara ya wafanyakazi kufuatia kucheleweshwa kwa usambazaji wa fedha kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.

BY NEWS DESK