Rais William Ruto leo hii ataitia saini kudhinisha kuwa sheria Mswada wa Nyumba za Makazi ya bei nafuu, sheria ambayo itarejesha makato ya ushuru wa nyumba.
Hafla hiyo ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika jana Jumatatu asubuhi iliahirisha ambapo taarifa kutoka Ikulu ilieleza kuwa rais atatia saini mswada huo hii leo.
Bunge la Seneti na Bunge la Kitaifa lilipitisha mswada huo wiki jana huku marekebisho yakiwasilishwa katika mswada huo ikiwa ni pamoja na kuzishirikisha serikali za kaunti na kuzijumuisha kwenye mpango huo.
Mswada huo umelenga kuwafanya wakenya wote wanaolipwa na wasiolipwa, walipe asilimia 1.5% ya malipo yao ya kila mwezi kwa hazina ya nyumba nafuu.
Tozo hiyo imekuwa na mgogoro mkubwa kati ya serikali, mahakama na wananchi huku wengi wakihoji mfumo wake wa kisheria.
Ikumbukwe kuwa Jopo la majaji watatu mwaka wa 2023 lilizuia ukusanyaji wa ushuru huo kwa msingi kwamba ulikuwa wa kibaguzi na ukiukaji wa moja kwa moja wa Kifungu cha 10 cha katiba.
Hapo awali magavana kupitia vikao vya ushirikishaji wa maoni ya umma waliibua maswali na wasiwasi wa kwa nini serikali ya kitaifa inatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba licha ya kuwa ni mpango uliogatuliwa.
Magavana sasa wataunda kamati za mawasiliano za kaunti ili kusimamia utekelezaji wa mpango huo.
BY MJOMBA RASHID