HabariNews

Mwanagenzi ‘Intern’ Anawezaje kuwa na Mshahara? Waziri Kuria Kusimamia Mikataba yote ya Makubaliano

Waziri wa Huduma na Utumishi wa Umma Moses Kuria amesema kuanzia sasa na kuendelea Wizara yake ndiyo itakayoongoza majadiliano ya Mikataba yote ya Makubaliano (CBA) na vyama vyote vya miungano ya wafanyakazi nchini.

Kauli yake Waziri Kuria inajiri wakati ambapo kizungumkuti cha mgomo wa madaktari wanaoshinikiza Serikali kutekeleza mkataba wa makubaliano yao ya mwaka 2017 kikiendelea kugubika taifa na kupelekea shughuli za huduma za afya kulemazwa katika hospitali za umma.

Kulingana na Waziri Kuria baadhi ya matakwa wanayoshinikiza madaktari yakiwemo mishahara ya 206,000 kwa madaktari wanagenzi (medical interns) kama ilivyobainishwa kwenye Mkataba wao wa Makubaliano hayafai kwani hayaendani na uwezo wa serikali kifedha.

Akihutubia wanahabari mnamo Ijumaa Aprili 12, Waziri Kuria alieleza kuwa iwapo serikali itaafiki matakwa hayo ya madaktari, basi itachochea vyama vingine vya wafanyakazi wa umma kushinikiza matakwa ambayo hayawezi kutekelezeka kamwe.

Kwenda mbele sasa, Wizara yangu pekee itakuwa ikiongoza majadiliano ya CBA kwa kuwa sisi ni wataalamu wa Serikali ya Jamhuri ya Kenya katika Masuala ya Uajiri (HR)…ili tuwe na mipangilio mwafaka na mfumo mzuri. Kwa sababu ukiangalia hili suala tuko nalo sasa kama mishahara ya madaktari wanagenzi…kwanza, vipi mwanagenzi anaweza kuwa na mshahara? Ni marupurupu/posho na si mshahara,” alisema Kuria akihutubia Vyombo vya habari.

Amesema hatua hiyo itapelekea udikteta katika taifa hivyo Kuria akibaini kwuepo haja ya kuweka majadiliano yote ya mikataba ya makubaliano kuwa chini ya usimamizi mmoja.

BY NEWS DESK