HabariNews

SRC Yakaza! Hakuna Nyongeza ya Mishahara kwa Wafanyakazi wa Umma kwa Sasa

Hakutakuwa na nyongeza ya mshahara ya kila mwezi kwa Wafanyakazi wa umma nchini kwa sasa na waajiri wanashauriwa kutotekeleza nyongeza yoyote.

Ni kauli yake Mwenyekiti wa Tume ya Kutathmini Mishahara na Marupurupu ya wafanyakazi wa Umma (SRC), Lyne Mengich, akizungumza mnamo Jumatatu katika Kongamano la 3 la Kitaifa kuhusu gharama ya Mishahara linaloendelea jijini Nairobi.

Mengich amesema ili kukabiliana na kupanda kwa gharama ya ulipaji mishahara nchini, hatua hiyo itaafiki kusaidia kufikia uendelevu wa fedha na maelewano, akiongeza kuwa taasisi zote zinapaswa kuhudumu ndani ya asilimia 50 ya kiwango cha kati katika kutoa mishahara na zile taasisi ambazo bado hazijafikia kiwango hicho zinapaswa kufanya hivyo kwa haraka iwezekanavyo.

Wakati uo huo Mengich amesema ili serikali iweze kupunguza kiwango cha fedha kinachotumiwa katika mishahara kutoka asilimia 46 hadi asilimia 35 kutahitajika mikakati kabambe ili kudhibiti ongezeko la mishahara nchini.

Hata hivyo akizungumza kwenye kongamano hilo Naibu Mwenyekiti wa Braza la Magavana Ahmed Abdullah amesema kwa sasa serikali za kaunti zinatumia asilimia 45 ya pesa zake kwa mishahara na kupunguza hilo haiwezekani kutokana na serikali kuu kuongeza kodi kwa waajiri kama vile kodi ya nyumba na bima ya afya kwa wote.

Kwa upande wake Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amewahimiza watumishi na wafanyakazi wa umma kuwa na Subira huku serikali ikijaribu kutafuta suluhu kwa hali ngumu ya uchumi inayoshuhudiwa.

Koskei amesisitiza kuwa ni sharti taifa liishi ndani ya uwezo wake wa kifedha ikizingatiwa kuwa serikali inakosa fedha za ziada kuwalipa wafanyakazi wa umma pia inapambana na mishahara ya juu ya wafanyakazi.

BY NEWS DESK