HabariNews

Rais Ruto Aaapa Kudhibiti Ongezeko la Ajali za Barabarani katika Utawala wake

Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wanaokiuka sheria za barabarani na kusababisha vifo na maejruhi.

Haya ni kulingana na rais William Ruto, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Usalama Barabarani wa 2024-208 katika Ukumbi wa KICC jijini Nairobi mnamo Jumatano Aprili 17.

Rais alisema ni sharti utepetevu na uzembe barabarani ukomeshwe na hatua za usalama kuimarishwa ikiwa ni pamoja na utumizi wa teknolojia za kisasa kufuatilia ukiukaji wa sheria za trafiki na kukabiliana na ufisadi barabarani.

“Kukwepa ukaguzi, kupuuza kutengeneza magari yawe salama, tabia ya uzembe barabarani na kutoa rushwa ili kuepuka uwajibikaji ni aina kubwa ya utovu wa nidhamu unaochangia, ambao lazima uadhibiwe,” alisema Rais.

Rais aidha aliapa utawala wake wa Kenya Kwanza utadhibiti kabisa ongezeko la jinamilizi la ajali za barabarani akisema ni sharti ajali zipungue kwa asilimia 50 akizishinikiza idara mbalimbali husika ikiwemo Wizara ya Uchukuzi ziwajibike la sivyo watajipata matatani.

Rais Ruto alitoa wito wa ushirikiano thabiti kati ya Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama(NTSA) na Idara ya Trafiki ya polisi katika utekelezaji wa mpango huo wa usalama.

Alisema mpango huo lazima usaidie kupunguza ajali, vifo na majeruhi kwa asilimia 50 katika mwaka mmoja ujao.

“Idadi ya ajali za barabarani lazima ipungue.  Ni matarajio yangu kuwa tutakuwa utawala utakaoshughulikia changamoto hii,” alisema.

Rais Ruto alisema hayo wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Usalama Barabarani 2024 -2028 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta jijini Nairobi.

BY MJOMBA RASHID