HabariNews

Jenerali Ogolla Kuzikwa Jumapili Aprili 21 Kaunti ya Siaya

Mkuu wa majeshi ya ulinzi nchini Jenerali Francis Omondi Ogolla atazikwa Jumapili hii huko kaunti ya Siaya.

Kulingana na familia Jenerali Ogolla atazikwa nyumbani kwake eneo la Nginya, Alego-Usonga kaunti ya Siaya.

Jenerali Ogolla alifariki hapo jana Alhamisi na wanajeshi wengine 9 kufuatia ajali ya ndege iliyotokea eneo la Sindar kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Kutokana na kifo cha jenerali huyo rais William Ruto alitangaza siku tatu za maombolezi ambapo bendera ya nchi, ya Afrika Mashariki na ile ya kijeshi zitapepeushwa nusu mlingoti hapa nchini na katika ofisi za ubalozi za Kenya mataifa mbalimbali.

Viongozi mbalimbali nchini na nje ya nchi wameendelea kutuma risala zao za rambirambi kuomboleza kifo cha Jenerali Ogolla.

Rais wa Tanzania Samia Suluh Hassan kupitia akaunti yake ya mtandao wa X ameeleza kuzipokea habari hizo kwa masikitiko makubwa na kuitakia familia na Wakenya wote faraja kwa msiba huo.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla na wanajeshi wengine tisa katika ajali ya helikopta iliyotokea leo katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet.” Aliandika.

Natuma salamu za pole kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Mheshimiwa @William Ruto wananchi wote wa Kenya, familia, ndugu, jamaa na marafiki wa wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo. Poleni sana. Mwenyezi Mungu azilaze roho za ndugu zetu hawa mahali pema peponi. Amina.”

 

Naye kiongozi wa Upinzani Raila Odinga amemtaja Ogolla kama mzalendo halisi aliyeitumikia taaluma yake vilivyo na kujitolea kulihudumikia taifa.

BY NEWS DESK