HabariNewsUncategorized

Shule Kufunguliwa Jumatatu Mei 13, Rais William Ruto atangaza

Rais William Ruto mnamo siku ya Jumatano Mei 8, alitangaza kuwa shule zote zitafunguliwa rasmi Jumatatu ya Mei 13 kwa shughuli za masomo ya muhula wa pili.

Akitoa tangazo hilo kwenye ikulu ya Nairobi wakati wa kikao na viongozi kutoka laikipia na Kajiado, rais alidokeza kupata ushauri kutoka kwa idara ya utabiri wa hali ya hewa ambayo kulingana naye mvua kubwa inayosababisha mafuriko nchini inaendelea kupungua.

Kadhalika Rais alikariri kuwa tayari serikali kuu imeweka mikakati ya ushirikaino na wabunge kupitia hazina ya Ustawishaji wa maeneo bunge NG-CDF kuhakikisha madarasa na miundo mbinu iliyoathirika katika shule zote nchini inakarabatiwa ili kuruhusu masomo kuendelea.

“Tumekubaliana kama serikali ya kwamba kwa sababu wale weather men wametuambia ya kwamba sasa mvua itazidi na kwenda chini na hatutaki watoto wetu pia wakose nafasi ya term ya kusoma.

         Ningependa kutangaza ya kwamba shule zote za Kenya zitafunguliwa Jumatatu ijayo.” Alisema Rais William Ruto.

Rais aliongeza kuwa wazazi wanafuata maagizo kutoka kwa seriklai na idara ya anga na kwamba kwa sasa wanafunzi watakuwa salama shule zitakapofunguliwa.

Kulingana na kalenda ya masomo ya mwaka 2024 shule zote zilikuwa zinafaa kufunguliwa kwa muhula wa pili Aprili 29, tarehe ambayo iliahirishwa kwa wiki moja hadi Mei 6 kutokana na athari ya mafuriko.

Hata hivyo kutokakana na athari ya mafuriko na mvua kubwa iliyokuwa ikishuhudiwa, serikali ililazimika kwa mara nyingine kuahirisha ufunguzi huo hadi tarehe isiyojulikana hadi pale hali itakuwa salama kwa wanafunzi kurudi shuleni bila ya kuathirika.

Awali serikali ilitangaza kwamba imetenga silingi bilioni 1 kwa ajili ya ukarabati wa miundo mbinu na shule zilizoathirika kote nchini ambapo takwimu za serikali zilionyesha kuwa zaidi ya shule 1,960 ziliathirika na mafuriko hayo.

BY MAHMOOD MWANDUKA