HabariNews

Wanawake Wajawazito Kupata Afueni kufuatia Kujengwa Kwa Zahanati ya Kujifungulia Kiwandani

Katika juhudi za kuhakikisha kuwa hakuna wanawake wajawazito wanaojifungua nyumbani ili kupunguza hatari ya wanawake hao kupoteza maisha, wakazi wa Kiwandani huenda wakapata afueni kufuatia ujenzi wa zahanati ya wanawake kujifungua kuanza rasmi.

Kwa mujibu wa diwani wa Sokoni Ray Katana Mwaro, ujenzi huo utakaogharimu shilingi milioni 12 na utakaochukua takriban miezi minane kukamilika kwake, utawezesha wanawake 6 kujifungua kwa wakati mmoja.

“Kupitia pesa za maendeleo ya wadi nimeweka pesa kima cha shilingi milioni 12 kujenga maternity ya kisasa ambayo itakuwa na vitanda 6 vya wanawake kujifungua kwa wakati mmoja pamoja na vitanda 6 vya wanawake kupumzika baada ya kujifungua. Na maternity yenyewe tunaijenga ya ghorofa mbili ama tatu ambapo tunatazamia chini ya miezi minane itakuwa ipo tayari, lakini tuko na imani itachukua muda mfupi.” alisema Mwaro.

Kwa upande wake muuguzi msimamizi katika zahanati ya Kiwandani Rebecca Kosgei amesema imekuwa changamoto kuwahudumia wanawake wajawazito zaidi ya elfu 2 wanaokwenda kujifungua zahanatini hapo kila mwaka kutokana na kukosekana kwa mahali maalum pa kuendeshea shughuli hiyo.

Amesema hali hiyo imechangia kupungua kwa idadi hiyo mpaka wanawake 40 wanaojifungua kwenye zahanati hiyo kila mwezi kutokana na ukosefu wa ubora wa huduma hiyo.

“Kwa hivyo ukilinganisha idadi ya wanawake 2,000 dhidi ya wauguzi wawili hiyo haiwezekani. Akina mama wengi huanza kliniki hapa kama 300 kila mwezi lakini ifikapo muda wa kujifungua utapata labda wanawake 30 hadi 40. Hali hii ilitufanya tukajiuliza pamoja na hawa wanawake nini ambacho huwafanya hamji zahanatini hapa wakati wa kujifungua? Wakasema hakuna mazingira mazuri ya sisi kujifungua.” alisema Kosgei.

Tumaini Fondo mkaazi wa Kiwandani ameeleza umuhimu wa ujenzi wa zahanati hiyo akisistiza kuwa kwa muda mrefu wanawake wamelazimika kutembea mwendo mrefu kutafuta huduma hizo.

“Mradi huu utasaidia kina mama wengi sana kwasababu huu mradi umechukuwa sehemu kubwa sana ambapo watu kutoka Kiwapa wakitaka kujifungua huwa wanakuja hapa, wengine kutoka Kibaoni wanakuja hapa kwasababu hospitali ya rufaa huwa kuna foleni ndefu. Kwa hivyo hili jingo litakapoisha tutapata kina mama wengi sana wakijifungua hapa ambapo imetusaidia hata kwa mambo ya nauli.” alisema Tumaini.

ERICKSON KADZEHA