HabariNews

USAFIRI WA MARA KWA MARA WA BODA BODA WATAJWA KUKWAMISHA ONGEZEKO LA WATU KILIFI

Sekta ya usafiri wa boda boda ikiwa imeajiri zaidi ya watu milioni tatu humu nchini tangu kuanza kwake, njia hiyo ya usafiri imetajwa kuwa ya rahisi na haraka. Licha ya usafiri huo kukumbatiwa na wengi, sasa usafiri huo unadaiwa kuchangia kutoongezeka kwa idadi ya watu kaunti ya Kilifi.

Kwa mujibu wa mbunge wa Kilifi kaskazini Owen Baya vijana wanaoingia kwenye maisha ya ndoa wamekuwa wakitaabika kupata watoto kutokana na kujihusisha na uendeshaji wa boda boda, huku wengine wakichukua muda mrefu kabla ya kuongeza watoto wengine.

Anasema hali hiyo imechangia kupungua kwa idadi ya watu kaunti ya Kilifi bila wengi kuwa na ufahamu wa hilo.

Utafiti uliofanywa na shirika Nature.com ukionesha kuwa asilimia 58 ya vijana wa kati ya umri wa miaka 20-29, asilimia 63 ya vijana wa umri kati ya 30-39 na asilimia 76 ya watu wenye umri wa miaka 40-49 wanaojihusisha na uendeshaji wa piki piki wa mara kwa mara wako katika hatari ya kukosa watoto.

“Vijana wadogo wanaoa hawapati watotona wakipata wanabaki kama miaka mitatu minne hivi kabla kupata mwengine na inaishia hapo. Wengi wakimaliza shule wanaingilia uendeshaji wa pikipikina zile pikipiki zinatoa joto kali sana ambalo linaaribu kizazi. Sasa idadi ya watu wetu inapungua hiyo ni sayansi, wale wamesoma sayansi wanatambua hilo.” alisema Baya.

Amewarai wazazi kuwashauri wanao kutafuta njia nyingine za kutafuta pesa badala ya kujiingiza kwenye sekta hiyo ya usafiri wa boda boda.

Aidha amewahimiza kutafuta msaada wa matibabu ili kujikinga na athari zinazotokana na uendeshaji wa mara kwa mara wa pikipiki.

“Sasa kila kijana akimaliza shule anakimbilia kwa uendeshaji pikipiki na hili sio kwa wanaume pekee hata kina mama na hiyo inaelezwa vizuri kwenye sayansi. Wewe unadhani ni jambo zuri lakini wewe unajiweka kwenye hatari. Kile ninachosema ni hivi ndugu zangu, tutafute njia nzuri ya kutafuta pesa.” alisema Baya.

 ERICKSON KADZEHA