HabariLifestyleNews

Kongamano La 41 la Taasisi ya Wahasibu Nchini (ICPAK) laandaliwa Mombasa

Spika wa Bunge la kitaifa Moses Wetangula amesema kuwa  mchango wa wahasibu ni muhimu katika kutathmini mapendekezo yaliyotolewa  na wananchi kuhusu mswada wa fedha wa mwaka 2024 ili kujumuisha yenye manufaa zaidi kwa taifa na wakenya kwa jumla.

Akizungumza katika ufunguzi rasmi wa kongamano la 41 la wahasibu hapa Mombasa, mnamo Jumanne Mei 21, Spika Wetangula aliweka wazi kuwa serikali inakumbwa na changamoto ya madeni inayochangia pakubwa kudorora kwa uchumi wa taifa huku akieleza kuwa bunge linafanya kadri liwezavyo kuhakikisha mipango ya serikali kwa wananchi inatimizwa.

Aidha Wetangula amewataka wahasibu kuhakisha hawajihusishi na sakata za ufisadi na ufujaji wa fedha za umma akisema kuwa matukio hayo huharibu mipango ya maendeleo iliyoelekezewa wananchi.

“Wahasibu wote nchini wanalo jukumu la kutathmini matumizi ya bajeti ya serikali hatua ambayo itasaidia pakubwa kungazia matumizi ya fedha za umma katika idara, sekta na wizara wote za serikali ya kitaifa na pia ya serikali ya kaunti.Kwa sasa taifa letu la Kenya, thamani ya shilingi inakabiliwa na changamoto ya madeni ya kigeni. Changamoto hizi zinahitaji mabadiliko ya vipengee tofauti vya ibara ya katiba ili kuangazia kwa kina pendekezo la mswada wa fedha wa 2024 ambao umezua na kuleta hisia mseto miongoni mwa wakenya.”

Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa Wahasibu nchini Nancy Gathungu ametaja masaibu wanayopitia wahasibu katika harakati ya kutekeleza majukumu yao ikiwemo vitisho pindi wanapojitenga na matukio ya kifisadi hususan ufujaji wa fedha katika mashirika mbalimbali akiwataka kutoingia mtegoni na wawe na uadilifu katika utendakazi wao.

Kadhalika ameongeza kuwa ukwepaji wa kulipa ushuru ni mojawapo ya vyanzo vya taifa kutofikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na serikali hali ambayo hulemaza ukuaji wa taifa.

“Taaluma ya uhasibu nchini inakumbwa na changamoto mojawapo ikiwa ni vitisho kwa wahasibu wetu wanaojitenga na matukio ya kifisadi. Ila nawahimiza wahasibu wote kusimama kidete na kuwa wadilifu katika utendakazi wao. Ufisadi unalemaza ukuaji wa taifa na huchangia kududumaa kwa miradi ya maendeleo.”

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Wahasibu wa Umma nchini(ICPAK) Philip Kakai amewataka wahasibu wote nchini kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuhakikisha wanaziba mapengo yote yanayotumika kama mianya ya kutekeleza ufisadi.

Vilevile amewahimiza wahasibu kujihusisha katika masuala yanayofungamana na uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikizingatiwa kuwa taifa limeathirika pakubwa kutokana na mabadiliko hayo.

“Matukio ya hivi karibuni yaliyolikumba taifa letu kama vile ukame, mafuriko ni athari ambayo imetokana moja kwa moja na kutolinda na kutunza mazingira yetu. Nawahimza sote tujitolee kutunza mazingira yetu kwa kupanda miti na kutunza mito na misitu.”

Kongamano hilo limeleta wahasibu mbalimbali kutoka kote nchini kujadili masuala yanayowaathiri na jinsi ya kuyatatua huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni mchango wa taaluma ya uhasibu katika ukuaji na maendeleo ya taifa.

BY ISAIAH MUTHENGI