HabariNews

Captain William Ruto Mashakani

Kamati ya Barabara,Usafiri na makazi kwenye bunge la Seneti ilisitisha na kuahirisha ghafla kikao cha pamoja cha  kuuhoji usimamizi wa Halmashauri ya Bandari nchini KPA.

Hatua hiyo ya kamati ya seneti iliafikiwa baada ya Mkurugenzi mkuu wa Halsmashauri hiyo William Ruto kususia kikao cha pamoja cha kamati hiyo kwa mara nyingine pasi kutuma hudhuru.

Kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti Paul Karungo Thangwa ambaye pia ni seneta wa kaunti ya Kiambu ilikataa katakata kuwasikiliza wawakilishi wa mkurugenzi huyo waliofika mbele ya kamati hiyo kwa niaba yake.

“Hakuna mawasiliano au heshima ya kumpigia simu mwenyekiti kumwambia kuwa hatafika mbele ya kamati.  Ni makosa kuwateua nyinyi kumwakilisha ila kwa kuwatuma labda kuwatuma huenda alifikiria kwamba anafanya vyema.hatua aliyoichukua si njema machoni mwa  seneti kwa sababu tungewasiliana ndipo tuelewe ni wapi pa kuanzia. Kama tungeambiwa yuko mahali  Naivasha jana tungesafiri kuenda tu kumsikiliza kwa sababu haya ni mambo makubwa na ni muhimu kufuatiliwa” Alisema Karungo

Kamati hiyo aidha imetoa makataa ya hadi Julai tarehe saba kwa  William Ruto kufika mbele yake vinginevyo haitakuwa na budi ila kumtoza faini ya laki tano mkurungenzi huyo au ichukue hatua ya kumwandikia barua inspekta mkuu wa polisi Japhet Koome  kushurutisha kukamatwa kwake ili kufikishwa mbele ya kamati hiyo.

“Hatuchukulii rahisi hatua yake ya kususia mwaliko wa kamati hii. Kamati hii ina mamlaka ya kuitisha mkutano naye tena iwapo atakikana kufika mbele ya kamati hii na pia ina mamlaka ya kumpiga faini ya takriban laki tano ambayo atalipa kutoka mfukoni mwake na si kutoka  kwa KPA.Hii kamati pia ina nguvu na mamlaka ya kumpa inspekta mkuu wa polisi barua ya kumkamata na kumleta mbele ya kamati hii.Tunamwalika tena na  asipofika sasa tutakuwa na uhuru wa kumchukulia hatua kwa mujibu wa sheria” Akaongeza Thangwa

Licha ya kikao cha leo kufeli kufanyika, maseneta hao wameshikilia msimamo wao kuwa sharti William Ruto afike mbele yao kuyajibu masuala tata kuhusu suitontofahamu iliyoko bandarini ya sakata, uongozi mbaya na ubadhirifu wa mali ya umma.

“na kwenye kikao kijacho hatuji Mombasa, atakuja Nairobi kwenye bunge la seneti kwa sababu ukiangalia madai haya hata bila Kwenda kwenye stakabadhi, ukiangalia ni masuala ambayo tukiyatathmini kwa kina huenda kuna sakata inayoendelea kwenye bandari ya dola milioni 2.5. Halmashauri ya bandari inawadai watu zaidi ya shilingi bilioni 5. Tulitaka mkurugenzi huyo mkuu kuwa hapa ndipo afafanue madai haya. Tunajua anaweza jibu hayo maswali lakini tunataka mwenyewe afike ayajibu madai na masuala mengine yanayoibuliwa bandarini” Alisema Karungo

Kauli ya kamati hiyo inajiri huku madai hayo sasa yakizidi kuibuliwa zaidi  eneo hilo nazo juhudi za kutafuta majibu mwafaka kutoka kwa Mkrugenzi huyo mkuu wa Bandari zikigonga mwamba.

BY EDDAH SITUMA