Mashirika ya kijamii kaunti ya Kilifi yametoa wito kuanzishwa kwa mazungumzo ya marika maarufu “Intergenerational conversation” ili kukabiliana na changamoto ya upotokwaji wa maadili katika jamii pamoja na kuondoa unyanyapaa kwa wasichana waliojifungua wakiwa na umri wa chini ya miaka 18.
Mashirika ya kijamii yanaendelea kuhimiza kuanzishwa kwa mazungumzo ya marika kwenye jamii ili kupambana na upotokwaji wa maadili hasa kuondoa unyanyapaa unaoelekezwa kwa kina mama wachanga.
Julius Kamoni mwanaharakati wa maswala ya jamii kutoka shirika la Society Empowerment & Emergency Mitigation SEEM, anasema maongezi ya marika yatasaidia kizazi cha sasa kupata wasia wa kimaisha kutoka kwa kizazi kilichotangulia.
Ameeleza kuwa changamoto zinazoendelea kushuhudiwa kwenye jamii zinatokana na mianya iliyopo kwenye jamii kwa kukosa kuona umuhimu wa kujadiliana kuhusu maswala ya ngono.
“Endapo hawa watoto watakungwaa waanguke basi ifahamike katika jamii kwamba aliyepotokwa wa kwanza ni mimi mzazi kabla tufike kwa yule mtoto. Ule muelekeo tunaochukua ni kutengeneza majadiliano ya marika watu wazima kuongea na watoto kina nyanya kuongea na wasichana na kina mama waliowazidi umri, mababu zetu kuongea na wavulana.
“Nyanya zetu kuwaweka pamoja na kuwapa ushauri kuhusu maswala ya ngono maana tusipo lijadili litatuangamiza.” alisema Kamoni.
Kamoni anasema licha ya serikali kujitahidi kuhakikisha utekelezaji wa haki ya elimu kwa kila mtoto bado kunao kina mama wengi wachanga hawajaweza kurudia masomo kutokana na kuogopa unyanyapaa kutoka kwa jamii huku, takwimu zikionesha kuwa kaunti ya Kilifi inaorodhesha asilimia 12.5 ya mimba za utotoni ikilinganishwa na takwimu ya kitaifa ambayo ni asilimia 12.
“Kwangu nasema ndio, serikali imefanya kazi lakini bado kuna nafasi kubwa ambazo bado zinahitaji kujazwa. Na ni muhimu zaidi kwamba tufungue nafasi kuwaruhusu wengi wao zaidi kurudi shule. Maana ndio wanarudi shule lakini pia wako wengi ambao wanabaki nyumbani sababu ya kuogopa unyanyapaa.
“Kilifi kwa sasa imesimama katika asilimia 12.5 katika maswala ya mimba za utotoni, Kenya nzima imesimama katika asilimia 12 hii inatuambia nini? Ni kwamba Kilifi tunadidimia, elimu isipoenda kwa mtoto wa kike jamii inaangamia.” alisema Kamoni.
Carol Israel mtetezi wa Haki ya Afya ya uzazi kaunti ya Kilifi kutoka shirika la ICRH, amesema wasichana wengi wamekuwa wakidhulumiwa kutokana na ukosefu wa ufahamu wa haki zao.
Amewataka wasichana na wanawake kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na viongozi tawala katika kutafuta haki zao kwenye jamii.
“Lakini utapata kina mama wetu wachanga huko mashinani wanaangukia kwenye mtego kwasababu hawana ufahamu. Kwa hivyo nitawaambia wanawake mahali popote walipo unalindwa na katiba ya taifa hili lakini pia simameni kidete jueni haki zenu pia mfahamu ni wapi pa kutafuta misaada ya maswala haya.
“Unaweza ukatutafuta sisi mashirika ya kutetea haki za binadamu ama hata viongozi tawala kama vile machifu ama mtu mwengine yeyote anayetetea haki za binadamu upate usaidizi.” alisema Israel.
Erickson Kadzeha