Huenda changamoto za huduma za matibabu zinazowakabili wakaazi wa eneobunge la Kisauni zikapata suluhu la kudumu kufuatia ufunguzi wa kitengo kipya cha upasuaji eneo la Utange.
Serikali ya kaunti ya Mombasa imefungua sehemu hiyo mpya ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Pwani (Makadara) katika eneo la Utange na ikitarajiwa kuwarihishia huduma wakazi sawia na kupunguza msongamano katika Hospitali Kuu ya Makadara kisiwani Mombasa.
Akizungumza mnamo Ijumaa Novemba 8 wakati wa ufunguzi huo Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir alisema Hospitali hiyo ya kiwango cha Level 4 itakuwa ya kwanza kushughulikia upasuaji wa tatizo la kupasuka midomo kwa watoto wachanga huku ikitarajiwa kuwafaidi wakazi wa eneo hilo na hata wa kaunti jirani ya Kilifi.
“Kuanzia kaunti ya Kilifi hadi Coast General hakuna hospitali ya umma inayoweza kufanya operation hii ndiyo ya kwanza katikati ya hapa, tumeanzisha tuwafanyie watoto upasuaji wale wenye shida yam domo wafanyiwe hapa nao waweze kutabasamu kama wengine.” Alisema.
Gavana Nassir aidha alisema ataendeleza mpango wa matibabu ya bure kwa watoto wa chini ya umri wa miaka 5 licha ya mabadiliko ya bima mpya ya afya kutoka NHIF hadi SHA akiagiza maafisa husika kulifanikisha hilo katika hospitali zote za umma katika kaunti hiyo.
“Tulikuwa na policy kila mtoto wa chini ya miaka mitano hospitali za kaunti zisiwatoze pesa. Nadhani baada ya kuingia hii mambo ya SHA na SHIF kukawa na suitofahamu wafanyakazi wa kaunti hakuweza kuelewa, sasa yale nimesema iweze kueleweka waziwazi hakuna mtoto yeyote wa chini ya miaka 5 ambaye ni wa Mombasa anastahili mzazi wake kulipishwa hata peni lolote katika taasisi zetu za afya za kaunti.” Akasema.
Wakati uo huo Nassir alisema serikali yake ikishirikiana na wawakilishi Wadi na maafisa wa afya wa nyanjani na viongozi wengine watafanya zoezi la usajili wa bima mpya ya afya ya SHA kwa wakazi wa Mombasa akisema serikali hiyo aidha itawalipia wasiojiweza.
By Mjomba Rashid