HabariLifestyleNews

Krismasi ya Huzuni Pwani; Watu 7 Wafariki katika Matukio Tofauti

Watu watatu wameaga dunia baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Mariakani, barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.

Inaarifiwa kuwa gari hilo mapema Jumatano Disemba 25, liliwagonga watu sita waliokuwa wakitembea kwa miguu katika eneo la Dam View baada ya dereva kushindwa kulidhibiti.

Watatu hao walioaga dunia ni wanaume wawili na mwanamke mmoja.

Wengine watatu waliojeruhiwa akiwemo dereva wanaendelea kutibiwa katika hospitali ya Mariakani huku miili ya waliofariki ikipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani (Makadara).

Gari lililosababisha ajali hiyo limepelekwa katika kituo cha polisi cha Mariakani huku uchunguzi ukiendelea.

Kwengineko, Biwi la simanzi limetanda katika kijiji cha Haroresa kaunti ya Tana River kufuatia vifo vya watoto wanne waliokufa maji.

Inaarifiwa kuwa watoto hao wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 13 walikufa maji walipokuwa wakiogelea katika kidimbwi kimoja cha maji kabla kuzama, Jumanne jioni.

Akithibitisha kisa hicho Kamanda wa Polisi kaunti ndogo ya Galledyertu Tana River David Lawendi amesema miili ya watoto imeopolewa katika maji na kutambulika.

Miongoni mwa waliofariki ni watoto watatu wa kike na mvulana mmoja.

Tayari miili ya watoto wote wanne wanaoaminika kuwa wanafunzi wa shule ya msingi ya Haroresa, imezikwa.

By Mjomba Rashid