Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Douglas Kanja na Mkurugenzi Mkuu wa DCI Mohammed Amin wamekaidi amri ya mahamaka iliyowaagiza kufika mbele yake kueleza waliko vijana 6 wanaodaiwa kutekwa nyara na maafisa wa polisi.
Badala yake Kanja na Amin mnamo Jumanne walituma mawakili wao mahakamani jambo lililowakera mawakili wa familia za vijana hao na pia mawakili wa Chama cha Mawakili, LSK.
Mawakili hao wakiongozwa na Kalonzo Musyoka, Martha Karua na Eugine Wamalwa wanataka Inspekta mkuu wa polisi ashtakiwe na makosa ya kukaidi matakwa ya korti kuhusiana na utekaji nyara wa vijana wanaokosoa serikali.
“Ni jambo la kuhuzunisha sana, na natumai Hakimu anamaanisha alichokisema kwa kuwapa nafasi ya mwisho kwa wakuu hawa waje mahakanai. Lakini ni lazima vijana hawa wapatikane kwanza na waletwe hapa mahakani.” Alisema Kalonzo.
Kinara wa Narc-Kenya Martha Karua ameitaka Mahakama kumwamuru Inspekta Mkuu wa polisi Douglas Kanja kufika mbele ya mahakama kueleza waliko Wakenya wanaodaiwa kutekwa nyara na maafisa wa polisi, huku akipinga maombi ya upande wa idara ya usalama ya kutaka mkuu huyo kupewa muda zaidi ili kutayarisha taarifa rasmi.
Karua anayewakilisha wanaharakati waliokamatwa siku Jumatatu katika maandamano ameeleza mahakama kuwa kitendo cha Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja kutohudhuria kikao cha mahakama kama alivyoagizwa ni madharau na kupuuza idara hiyo.
Kwa upande wake Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa aidha ameitaka mahakama liwe liwalo kuwashinikiza wawili hao kufika mahakamani kuwawasilisha vijana hao mbele ya mahakama.
BY NEWSDESK