Mahakama ya Mombasa imewaachilia huru kwa dhamana ya shilingi 5,000 watu 13 wakiwemo wanaharakati waliokamatwa mnamo Jumatatu mjini Mombasa.
Watu hao walikamatwa wakati wakishiriki maandamano ya kupinga visa vya utekaji nyara wa vijana wakosoaji wa serikali na ukiukaji wa haki za kibinadam.
Mbele ya Hakimu Mkuu Rita Orora wamekanusha madai ya kufanya maandamano pasi kibali na hivyo kuachiliwa kwa dhaa hiyo ya shilingi 5,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.
Miongoni mwa wanaharakati hao waliofikishwa kortini ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Vocal Africa Hussein Khalid, Mathias Shipetta wa Haki Afrika, Tom Kazungu, Walid Skettty, Royal Khamisi, Catherine Khabuya, Lydia Adhiambo miongoni mwa wengine.
Kesi hiyo itatajwa tena Februari 12 mwaka ujao.
Huku hayo yakijiri, Seneta wa Busia Okiya Omtatah na waandamanaji wengine 22 waliokamatwa jijini Nairobi siku ya Jumatatu wameachiliwa kwa dhamana.
Seneta huyo na wanaharakati wenza waliokamatwa wameachiliwa kwa dhamana ya shilingi 1,000 na mdhamanini wa kiasi sawa na hicho.
Awali walikuwa wamewekea dhamana ya shilingi 50,000 na mdhamini sawa na kiwango hicho dhamana ambayo baadaye ilipunguzwa hadi shilingi 1,000 kila katika ishara ya nia njema kwa Mwaka Mpya.
By Mjomba Rashid