HabariNewsSiasa

Serikali Kufadhili Wabunge 4 Pekee Kwenda Ethiopia Kuunga Mkono Uchaguzi wa Odinga, AUC

Serikali itagharamia tu gharama za usafiri za wabunge wanne pekee kwenda Addis Ababa, Ethiopia Kumuunga mkono Raila Odinga.

Ni kauli yake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula akihutubia Bunge kikao cha Alhamisi.

Wetangula amefichua kuwa zaidi ya wabunge 40 walikuwa wamewasilisha maombi ya kutaka ufadhili wa kusafiri hadi Addis Ababa, kumuunga mkono Odinga kabla ya uchaguzi wa Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) siku ya Jumamosi.

Wabunge ambao watalipiwa gharama zao ni pamoja na; Nelson Koech (Mbunge wa Belgut na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi, Upelelezi na Mahusiano ya Kigeni) na Lydia Haika (Mwakilishi wa Wanawake wa Taita Taveta na Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Diaspora na Wafanyakazi wa Wahamiaji).

Bashir Abdullahi (Mbunge wa Mandera Kaskazini na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi, Ujasusi na Uhusiano wa Kigeni) pamoja na Mbunge wa Suba Kaskazini na Kinara wa Wachache Millie Odhiambo watafadhiliwa na serikali.

Kauli ya Wetangula inajiri huku kukiwa na ukosoaji mkubwa wa matumizi makubwa ya serikali, haswa kuhusiana na safari za nje.

Itakumbukwa kuwa mnamo siku ya Jumatano, Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi alitetea madai ya wajumbe wengi wa Kenya waliofika jijini Addis Ababa kuunga mkono Odinga kabla ya uchaguzi huo wa Jumamosi ikizingatiwa nia ya Kenya ya kunyakua Uenyekiti wa AUC.

Alipuuzilia mbali madai ya Kenya kutuma ujumbe mkubwa kupita kiasi ikilinganishwa na mataifa mengine akisema Serikali inajali hali ya kiuchumi.

Licha ya kuwa hakutoa nambari maalum ya wajumbe, Mudavadi alisema wajumbe hao, wanaotarajiwa ni pamoja na maofisa kutoka Wizara yake ya Mambo ya Nje na wajumbe wa Urais, huku akidai kuwa wajumbe wengine walifika huko kwa ufadhili wao binafsi.

Rais Ruto na mimi ni Waziri wa Masuala ya Kigeni. Na tunao maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ambao wanaunga mkono mchakato huu na tuna misheni hapa… tuna wajumbe konda wanaokuja hapa,” alisema.

Odinga mwenye umri wa miaka 80 atamenyana na, Richard Randriamandrato mwenye miaka (65) kutoka Madagascar na Mohamoud Youssouf wa Djibouti mwenye umri wa miaka (60).

Mgombea atakayefaulu atamrithi Moussa Faki wa Chad ambaye ataondoka baada ya uongozi wake wa mihula miwili ulioanza 2017 kukamilika.

By Mjomba Rashid