HabariLifestyleNews

Katibu wa baraza la mawaziri kaunti ya Kilifi azuiliwa kuingia ofisini.

Fujo zimeshuhudiwa katika ofisi ya katibu wa baraza la mawaziri na kaunti ya Kilifi Martin Mangi Mwaro baada ya vijana na baadhi ya wawakilishi wadi kumzuia katibu huyo alipojaribu kuingia ofisini kufuatia agizo la mahakama kumrejesha kazini.

Takriban wiki moja na nusu tangu katibu wa baraza la mawaziri na aliyepia mkuu wa utumishi wa umma kaunti ya Kilifi Martin Mwangi Mwaro kusimamishwa kazi, agizo la mahakama la kumrejesha kazini limeonekana kupuuzwa baada ya vurugu kuzuka baadhi ya vijana na wawakilishi wadi wakimzuia katibu huyo kuingia ofisini.

Kulingana na Mwaro licha ya kuwa na majadiliano ya amani na mshauri wa maswala ya sheria wa gavana wa Kilifi kuhusu kuzuiliwa kwake kuingia ofisini kuwasili kwa wakilishi wadi hao kumechangia kuzuka kwa vurugu hilo na kupelekea yeye kusukumwa nje ya ofisi akidai hatua hiyo ni ukiukaji wa agizo la mahakama.

“Baadae kukaja mshauri wa maswala ya sheria wa gavana wa KIlifi na tukaanza mazungumzo kuelezana kuhusu hatma ya agizo la mahakama nililokuwa nalo. Katika hali hiyo ya kujadiliana kukaingia viongozi wanasiasa ambao waliingia kwa fujo wakidai nitolewe ndani ya ofisi. Na wakafuatwa na nadhani wahuni ambao walileta vurumai pale mwishowe ndio nikaanza kusukumwa nikitolewa nje ya ofisi ambapo nilikuwa nimeamriwa na korti nirudi kulengana na sheria.” alisema Mwaro.

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti ya Kilifi Ibrahim Matumbo ametoa onyo kwa katibu huyo wa baraza la mawaziri dhidi ya kuonekana kwenye ofisi za serikali ya kaunti ya Kilifi hadi pale uchunguzi wa madai ya ufisadi dhidi yake utakapokamilika.

“Na mimi nataka kumwambia Mwaro aliyekuwa katibu wa baraza la mawaziri kwamba sisi tumenyamaza hatujaongea lakini sasa tumeona afadhali tuongee. Mimi nataka kukutahadharisha kwamba umefanya kitu kibaya sana na saa hii mimi kama kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Kilifi ndio natoa onyo kama kuna serikali yoyote inaweza kupambana na mimi. Nasema kwamba ofisi yoyote ya serikali ya kaunti ya Kilifi hatutamruhusu Mwaro aingie. Na akionekana sisi tutapambana na yeye.” alisema Matumbo.

Aidha Mwaro amejitenga na madai ya ufisadi anayoshutumiwa nayo huku akipuuzilia mbali onyo hiyo akisistiza kuwa ana haki ya kutafuta huduma katika ofisi hizo kama wananchi wengine.

“Sihusiani na ufisadi kwa hali yoyote ile lakini nilipoenda kortini, korti iliangalia na kuona sababu zilizotolewa mimi kuondolewa ofisini hatua inayostahili kisheria haikufuatwa. Licha ya kuhudumia wananchi nina haki kama mwananchi wa kaunti ya Kilifi kwenda kwa ofisi yoyote ya serikali kutafuta huduma, ushauri, ama mambo mengine ambayo yanaweza kupatikana kupitia ofisi ya serikali. Na sidhani kisheria iwapo mtu yeyote anahaki ya kunizuia kwenda kwa ofisi ya serikali.” alisema Mwaro

Erickson Kadzeha.