Polisi imesema imemkamata mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya katika eneo la Mnarani akiwa na misokoto 261 ya bangi inayokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi 52,200 pamoja na shilingi 13,400 pesa taslim zinazoaminika kuwa zimetokana na ulanguzi wa dawa hizo.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi eneo bunge la Kilifi kaskazini Stanley Tonui polisi wamefanikiwa kumtia mbaroni Pamela Atieno baada ya kupewa taarifa na umma kuhusu shughuli ya ulanguzi wa dawa za kulevya iliyokuwa ikiendelea nyumbani mwake.
Hata hivyo ameendelea kuwarai wananchi kupiga ripoti kwa polisi wakati wowote ulanguzi wa dawa za kulevya unapofanyika pamoja na biashara nyingine haramu ili kukomesha biashara hizo ambazo zimekuwa zikiendelea kuwa na madhara katika jamii.
“Tumepewa taarifa na umma kwamba eneo la Mnarani kuna mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya kwa jina Pamela Otieno. Na maofisa kutoka kwa kituo cha polisi cha Kilifi wakafika na kufanya msako nyumbani kwake na kufanikiwa kuapata misokoto 261 ya bangi yenye thamani ya shilingi 52,200 na shilingi 13,400 pesa taslim ambazo zinaaminika kuwa zimetokana na mauzo ya dawa hizo za kulevya.” alisema Tonui.
Ameongeza kuwa kuna baadhi ya maeneo kama vile Mnarani, Mtondia na Chumani ambayo yamekuwa yakiorodheshwa kuwa na visa vingi vya biashara ya ulanguzi wa dawa za kulevya huku akitoa onyo kali kwa wote wanaojihusisha na biashara hiyo kuwa sheria haitowasaza.
“Kuna mahali sisi kama baraza la usalama eneo hili tumeyaorodhesha kama vile Mnarani, Mtondia na Chumani ambayo yanawatu wengi wanaojihusisha ambao wanajihusisha na hizi dawa za kulevya lakini kile kitu ambacho nawahakikishia watu wa hapa Kilifi tutahakikisha wote ambao wanahusika tumewashika na tumewapeleka kortini na hatua ichukuliwe kulingana na sheria.” alisema Tonui.
Erickson Kadzeha.