Wakazi wa Mombasa waliotimu umri na kuafikia vigezo hitajika sasa wanahimizwa kujitokeza kujisajili kupata vitambulisho vya kitaifa kwa haraka iwezekanavyo.
Haya yanajiri huku idadi kubwa ikijitokeza katika zoezi la usajili wa umma kwa vitambulisho vya kitaifa lililoanza rasmi siku ya Jumatano.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mpango maalum wa utoaji huduma za kupata vitambulisho unaofanywa na serikali ya kaunti ya Mombasa Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir amesema nia na madhumuni ya mpango huo ni Kuhakikisha waliopoteza stakabadhi hizo za kitaifa wamezipata Kwa urahisi.
Nassir amesema serikali ya Kaunti itawalipia waliopoteza stakabadhi hizo ili Kuhakikisha Kila Mmoja amepata Kitambulisho chake.
“Zoezi hili tumezindua leo tarehe 7 na litaenda kwa wiki mbili likifanyika katika sub county zote, wadi zote 30 za kaunti ya Mombasa. Niwahakikishie kaunti itagharamikia kila kitu kwa aliyepoteza kitambulisho na ana apply kupata kingine, na yule anayeanza mwanzo kupata ID.” Akasema Gavana Nassir.
Naye kamishna wa kaunti hiyo Mohammed Noor amesema stakabadhi hiyo ni muhimu kwa kila mmoja kuwa nayo hasa kwa katika masuala ya Kutafuta ajira kwa vijana, Upigaji wa Kura na matumizi mengine Katika elimu ya juu haswa vyuo vikuu na taasisi nyinginezo.
Kwa upande mratibu Mkuu wa usajili wa Vitambulisho ukanda wa Pwani John Mutinda Kisula amesema kuwa watahakikisha kwamba Kila Mkenya aliyehitimu umri wa kupata Kitambulisho anafanikiwa kukipata popote alipo.
Kulingana na Mutinda, zoezi hilo limeanzia Mombasa na baadaye watazuru Katika Kaunti nyingine za ukanda wa Pwani ambapo wanaojisajili kwa sasa pia wataweza kutapata Maisha Card.
Haya yanajiri huku Idadi kubwa ya watu wasio na vitambulisho vya kitaifa ikishuhudiwa siku ya kwanza ya utoaji wa huduma hizo kaunti ya Mombasa ambapo wengi wao wakiwa ni wale waliopoteza stakabadhi hiyo muhimu na wengine wakiwa wale wanaosaka kitambulisho kwa mara ya kwanza.
Mwaka Saidi Babu ni Chifu wa eneo la Tudor eneobunge la Mvita.
Itakumbukwa kuwa Rais William Ruto alitangaza kufutilia mbali suala la ukaguzi wa vitambulisho hasa kwa wakazi wa maeneo ya mipakani mwa taifa, huku ikitarajiwa kuwa vijana wengi wa kizazi cha Gen Z watazidi kujitokeza kuchukua stakabadhi hiyo tayari kujiandaa kwa usajili na kushiriki wa uchaguzi mkuu wa 2027.
By News Desk