HabariNews

Kampeni Ya Kumi Dhidi Ya Muguka Yaanza Rasmi Kilifi

Kampeni ya siku kumi kupinga muguka imeanza rasmi mjini Kilifi, mashirika mbali mbali ya jamii pamoja na viongozi wakijitokeza kushiriki kampeni hiyo itakayotamatika tarehe 20 mwezi huu ili kushinikiza usitishwaji wa uuzaji wa muguka kaunti ya Kilifi.

Viongozi ukanda wa pwani wakiendelea kushilikia msimamo wao wa kuunga mkono marufuku ya utumizi na uuzwaji wa muguka kaunti ya Kilifi, mchakato huo unazidi kupata uungwaji mkono kutoka kwa mashirika mbali mbali ya jamii ambayo yamejitokeza kushiriki kampeni ya siku kumi dhidi ya muguka.

Kulingana na mbunge wa Kilifi kaskazini Owen Baya kampeni hiyo inalenga kuweka wazi kutokubalika kwa utumizi wa mmea wa muguka anaodai kuwa una madhara mengi ya kiafya pamoja na kuhatarisha kizazi kijacho.

Baya hata hivyo amewasihi wakazi kupiga ripoti kwa idara husika wanapoona shughuli za uuzaji wa muguka unaendelea ili kukabiliana vilivyo dhidi ya utumizi huo katika jamii.

“Sisi kama wananchi wa Kilifi tunataka nini? Hilo ndilo swali tunalofaa kujiuliza. Ndio nikasema tunatangaza siku kumi za uanaharakati dhidi ya muguka.

“Na ndani ya siku kumi hizi ningependa kuona mambo kadhaa yakifanyika kutoka kwa makundi ya kina mama, vijana na mashirika ya jamii washiriki maandamano ili name nikisimama kule bungeni kutoa hoja dhidi ya muguka waone kweli kuna kitu kimefanyika huku.” alisema Baya.

Kwa upande wao wanaharakati wametoa wito kwa serikali ya kaunti na viongozi wa kidini kuendeleza kampeni dhidi ya utumizi wa mihadarati katika maeneo yao.

Hata hivyo wamewataka viongozi kushirikiana katika vita hivyo ili kuhakikisha kuwa wanatokomeza utumizi, uuzaji na usambazaji wa mugoka katika kaunti ya Kilifi hadi lalama zao zitakaposikizwa na rais dkt. Wiliam Ruto.

“Wacheni wakimaliza kuimba wimbo wa taifa na sisi tunaimba wimbo wetu dhidi ya muguka. Wacha iwe akilini kwamba hatuutaki muguka mpaka waushike huo wimbo. Tuwe na mabango tuyabandike kila mahali kwamba hatutaki muguka ili wajue kweli sisi tumesema.

“Serikali ya kaunti ya Kilifi inafaa kuweka sheria kwamba muuzaji wa muguka akishikwa afungwe miaka kumi gerezani.

“Lakini je, tutawezaje kukabiliana na hili? Nafahamu kwamba serikali iko na taasisi za ujasusi basi wachunguze ni wapi ambapo muguka unaingilia hapa kaunti ya Kilifi wazibe huo mwanya.” walisema wakazi.

Ikumbukwe marufuku ya utumizi na uuzaji wa muguka ukanda wa  pwani yametolewa katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Taita Taveta.

ERICKSON KADZEHA.