HabariNews

Wizara ya Utalii Yahakikishia Wageni Usalama wa kutosha Nchini

Waziri wa Utalii na Wanyamapori Dkt. Alfred Mutua alieleza kwamba Kenya iko wazi na salama kwa wageni na wafanyabiashara licha ya matukio ya hivi karibuni ya machafuko.

Alisema Sekta ya Utalii na Wanyamapori imeajiri vijana asilimia 80, na machafuko hayo yanayosababishwa na maandamano ya kuipinga serikali yanaweza kusababisha kupoteza kazi na hata kusitisha fursa za ajira.

Kulingana na Waziri Mutua, Sekta ya utalii ilichangia shilingi bilioni 353 mwaka jana 2023 wakati ikilenga kuingiza shilingi bilioni 700 kila mwaka.

Aliongeza kuwa idadi ya wageni iliongezeka kutoka milioni 1 hadi milioni 2 mwaka 2023 wizara ya utalii ikitarajia takriban watalii milioni 3 mwishoni mwa 2024.

“Ni sekta ambayo inaezakuwa na shauku kidogo ikiwa nchi ina matatizo. Tumebahatika sana ya kwamba miaka ambayo imepita tulikuwa tunapata watalii milioni 1 mwaka uliopita tumefikia milioni 2.

Mwaka huu tunafanya kazi sana ndio tuweze kuwapata watalii milioni 3,” alisema Waziri Mutua.

Zaidi ya hayo Mutua alibaini kwamba utalii unategemea pakubwa usalama na amani ya nchi.

Hata hivyo, alihoji kuwa licha ya matukio ya hivi majuzi ya maandamano na ukosefu wa utulivu nchini, sekta ya utalii ingali imara.

“Tunataka kuwaambia kwamba wacha waje, ya kwamba hapa nchini Kenya tumeweka mikakati ya usalama…alisema.

Aliwahakikishia wageni wote humu nchini kwamba mikakati kabambe ya kiusalama imewekwa kwa watalii kuzuru maeneo yote nchini wanapoendelea na mipango yao ya kutembelea taifa la Kenya hasa maeneo ya mandhari ya Pwani.

Tumeweka mikakati kabisa ya usalama kuimarisha ya kwamba watalii wanakuja pwani, ndege zote zaa kuenda Mombasa, Diani tunaona bado ziko. Zile ndege zinatoa watalii kule nga’ambo bado zinakuja, na tunataka tuwe katika hali ya utulivu ndio watalii waje,” aliongeza.

BY NEWSDESK