HabariMombasaNewsSiasa

Sisi ndio wenye uwezo wa kutoa mwelekeo mwafaka wa kisiasa humu nchini, USP-K.

Vyama vya kisiasa vikiendeleza mikakati ya kuimarisha ufuasi na ushawishi wao kama njia ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao 2027, chama cha Umoja Summit Party of Kenya USP-K kimeeleza kuwa ndicho chama pekee kilicho na uwezo wa kutoa mwelekeo mwafaka wa kisiasa humu nchini.

Chama cha Umoja Summit Party of Kenya USP-K kimeeleza kuwa kinaendeleza mikakati ya kujiimarisha vilivyo na kutoa mwelekeo mwafaka wa kisiasa ili kupata nafasi ya kuwakwamua wakenya kutoka kwa uongozi usio bora.

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa chama hicho Barack Muluka wanalenga kutoa hamasa ya kutosha kwa wananchi jambo wanalodai litawapa uungwaji mkono watakapo simamisha wagombea wa nyadhifa mbali mbali za uongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Muluka aidha ameongeza kuwa chama cha USP-K hakitashiriki miungano ya vyama vya kisiasa kwani kuna mkinzano wa maono kati ya chama hicho na miungano mingine ya kisiasa.

“Tuna wasiwasi na yale mambo yanayoendelea humu nchini, tunajua hali ya taifa sio nzuri ila kwa sasa tunataka kulihakikishia taifa kwamba kama chama cha Umoja Summit Party of Kenya tunakwenda kutoa mwelekeo wa kisiasa humu nchini. Kupitia juhudi hizo kama chama tutaanza kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027 na tutasimamisha wagombea kwa kila wadhifa kama inavyoruhusiwa kwenye katiba yetu ya mwaka 2010.” alisema Muluka.

Naibu katibu mkuu wa chama hicho Naomi Sidi Kumbatha amesema kuwa chama hicho kitaanza mchakato wa kuwaandikisha wanachama na wagombea kote nchini, akisistiza kuwa wakazi watakuwa na nafasi ya kurekebisha hali ya taifa ya sasa iwapo watajiandikisha kuwa wanachama wa vyama vinavyowapa kipaumbele wananchi.

Ujumbe mkubwa ambao tuko nao ni ule ujumbe wa kuwasajili wanachama na wagombea wa nyadhifa mbali mbali kwenye chama chetu. Na tutasimamisha wagombea kutoka kwa nafasi ya uraisi kwenda hadi kwa mwakilishi wadi. Ningependa kuwarai wananchi na wagombea wajiunge nasi sasa hivi katika safari yetu ya kulikwamua taifa letu.” alisema Sidi.

Hayo yamejiri wakati wa kikao cha kamati ya kitaifa ya chama cha USP-K kupanga mkakati wa kuendesha zoezi la kuwaandikisha wanachama na wagombea kilichofanyika mjini Kilifi.

Erickson Kadzeha.