Maadhimisho ya Tamasha la Kitamaduni ya jamii ya Mijikenda maarufu Chenda Chenda yamefikia kilele chake huku jamii hiyo ikihimizwa kukumbatia utamaduni wao kujinufaisha.
Tamasha hilo lililoandaliwa katika eneo la Kayafungo, eneobunge la Kaloleni kaunti ya Kilifi limeshuhudia mwembwe na miondoko ya kila aina kuanzia kwenye mavazi, vifaa na vyakula vya kiasili.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria wamehimiza umoja na mshikamano sawia na kutumia fursa hiyo kuuza tamadauni ya jamii hiyo maeneo mengine ya nchi.
Awali akizungumza na wanahabari aliyekuwa Waziri wa Jinsia na Turathi Aisha Jumwa alieleza umuhimu wa maadhimisho hayo na kwamba tamaduni za jamii za Mijikenda katika mavazi, raslimali na vyakula vinaweza kutumiwa kama kitega Uchumi cha jamii hizo.
Hata hivyo licha ya wito wa umoja wa jamii ya Mijikenda siasa zimechukua usukuni huku viongozi wengine wakishindwa kuvumilia joto lake.
Aisha Jumwa alilazimika kusitisha hotuba yake na kuapa kuvuruga mkutano huo baada ya kuzomwa na wafuasi wa gavana Mung’aro.
Aisha Jumwa na Waziri wa biashara, Salim Mvurya, baadaye walilazimika kuondoka katika hafla ya Chenda Chenda baada ya kuzimiwa kipaza sauti kutokana na tofauti za kisiasa baina ya Jumwa na gavana Mung’aro.
Wakati uo huo Waziri wa Biashara na Viwanda Salim Mvurya amesema Serikali inapania kutumia kima cha shilingi bilioni mbili kununua ardhi kutoka kwa wamiliki wa vipande vya ardhi ukanda wa Pwani ambao hawaishi hapa, ili kuzinufaisha jamii halisi za eneo hili.
Amesema hatua hiyo inalenga kumaliza uskwota eneo hilo huku akiwataka wakaazi eneo hilo kuunga mkono miradi ya serikali ili waweze kunufaika na miradi ya serikali.
Wakati uo huo Mvurya amewataka wenyeji kukoma siasa za fujo, badala yake waungane kukuza tamaduni zao na kuzihifadhi kwa minajili ya kunufaika kimaendeleo.
Viongozi wengine waliohudhuria Tamasha hilo ni pamoja na Spika wa Bunge la Seneti, Amason Jeffa Kingi, Gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro na Naibu wake Flora Chibule, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir na Naibu wake Francis Thoya, Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kilifi Getrude Mbeyu na Zamzam Mohammed (Mombasa) Wabunge Owen Baya (Kilifi Kaskazini) Amina Mnyazi (Malindi), Paul Katana (Kaloleni), Harrison Kombe (Magarini) na Spika wa Kilifi Teddy Mwambire miongoni mwa viongozi wengine.
BY NEWS DESK