MichezoSports

Beatrice Chebet na Emmanuel Wanyonyi Wang’aa Kwenye Tuzo Za SOYA 2024

Mabingwa wa olimpiki  Emmanuel Wanyonyi  na Beatrice Chebet ndio mfalme na malkia wa tuzo za Soya baada ya kutwaa tuzo za Mwanaspoti bora wa mwaka 2024 upande wa wanaume na wanawake katika makala ya 21 ya tuzo za hizo  zilizoandaliwa katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano, KICC usiku wa Alhamisi.

Mwaka 2024 ulikuwa wa kufana kwa Chebet ambaye alifungua msimu wake kwa kutetea taji lake kwenye mashindano ya dunia ya Cross Country na baadaye kuivunjilia mbali rekodi ya dunia katika mbio za mita 10,000 kwenye mashindano ya Prefontaine Diamond League kabla ya kufunga mwaka na dhahabu mbili katika mashindano ya Olimpiki ya Paris alipoibuka kidedea kwenye mbio za mita 10,000 na 5,000 mtawalia.

Naye Wanyonyi aliandikisha rekodi  katika mbio za mita 800 na kunyakua dhahabu kwenye  mashindano yake ya kwanza ya Olimpiki kule Paris na kisha kuongezea ushindi huo na taji la kwenye Diamond League.

Samson Ojuka aliyeshinda nishani ya fedha kwenye mashindano ya olimpiki ya kuruka mapana alitwaa tuzo la mwanaspoti bora kwa wanariadha wanoishi na ulemavu upande wa wanaume huku Michelle Chepng’etich akinyakua tuzo hiyo upande wa wanawake.

Kocha wa timu ya soka ya kina dada junior starlets Mildred Cheche aliteuliwa kuwa kocha bora wa mwaka nayo timu yake ya Junior starlets ya wachezaji wasiozidi miaka 17 ikipokezwa tuzo ya timu bora  upande wa wanawake baada ya kutinga vitabu vya historia kwa kuwa timu ya kwanza ya soka nchini kushiriki kombe la dunia.

Nafasi ya timu bora ya upande wa wanaume ilichukuliwa na timu ya vikapu ya Nairobi City Thunder.

Katika upande wa shule mabingwa wa raga ya wachezaji 15 mwaka jana All Saints ya Embu walipokezwa tuzo ya shule bora upande wa wavulana nayo timu ya voliboli ya shule ya upili ya wasichana ya Kesogon ikatwaa ubora upande wa wasichana.

Tuzo ya Kocha bora wa shule ilichukuliwa na kocha wa shule ya upili ya All saints Benson Mwenda huku mchezaji mkongwe wa Gor mahia na Timu ya taifa Harambee Stars  John Bobby Ogolla maarufu ‘6 million dollar man’ akipewa heshima yake na kuingizwa katika ukumbi wa umaarufu wa SOYA, ‘hall of fame’.

 

By Mohammed Mwajuba