HabariKimataifaNews

Wanahabari Wausiwa Kukumbatia Teknolojia ya AI kwa Umakini Kuhakiki Kazi zao

Waandishi wa habari wameshauriwa kuwa waangalifu kwenye kazi zao za uandishi hususani wakati huu ambapo matumizi wa teknolojia ya Akili Mnemba (AI) yanazidi kushamiri kwa kasi nchini.

Kutokana na kuenea kwa kasi matumizi hayo hasa miongoni mwa vijana nchini, wanahabari sasa wakitakiwa kukumbatia teknolojia hiyo kwa uangalifu ili kuhakiki matukio na taarifa wanazoangazia.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari mratibu wa baraza la vyombo vya habari ukanda wa Pwani Maureen Mudi amesisitiza kwamba japo Akili Mnemba inasaidia ni jukumu la mwandishi habari kuitumia kwa uwajibikaji.

Kwa kuwa kuna AI si vibaya kuikumbatia lakini kwa kuzingatia maadili ya uanahabri. Wanahabari tuiongoze AI na sio vinginevyo. Tuzingatie nidhamu na itusaidie kuhakiki kazi zetu.” Akasema.

Wakati uo huo Mudi amedokeza kuwa kwenye takwimu za mwaka 2025 zilizotolewa na shirika la Reporters Without Border, Kenya imedorora katika uhuru wa vyombo vya habari ikiwa nambari 117 kwenye jumla ya 180.

Amesema ni ishara mbaya sasa ikizingatiwa mwaka uliopita kiwango cha Kenya katika kuzingatia uhuru kilikuwa nafasi ya 102 akithibitisha kuwa uhuru wa vyombo vya habari humu nchini umekiukwa kwa kiwango kikubwa hasa baada ya kushuka zaidi.

Kwa mwaka shirika la lilitoa orodha ya viwango vya mataifa yanayochunga uhuru wa wanahabari na Kenya imeshuka kutoka 102 hadi nafasi ya 117 na hii inaashiria nini; inaashiria nkuwa hali sio shwari,” akasema Mudi

Kwa upande wao watetezi wa haki za kibinadamu kaunti ya Mombasa wamewarai waandishi habari kushirikiana na mashirika hayo ili kuangazia kwa ukamilifu visa vya ukiukija wa haki za kibinadamu katika jamii.

Hawa hapa ni Francis Auma wa shirika la Muhuri na mwenzake Mathias Shipeta wa HAKI Afrika.

Haya yanajiri huku maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Wanahabari Duniani yakiendelea kufanyika nchini baada ya siku yenyewe maalum kuadhimishwa kila tarehe 3 mwezi Mei kila mwaka.

Wanahabari wa Sauti ya Pwani FM wakiongozwa na Mhariri Mkuu Mjomba Rashid walijumuika na wanahabari wengine kuadhimisha Siku hiyo ya Uhuru wa Wanahabari Duniani maadhimisho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Little Theatre.

By Mjomba Rashid