HabariNewsSiasa

Viongozi Wa Kanisa Katholiki Washinikiza Serikali Kukomesha Visa vya Utekaji Nyara na Ufisadi

Na huku visa vya utekaji nyara na kuchukuliwa watu kwa nguvu vikiendelea kushuhudiwa, viongozi mbalimbali wamejitokeza kukemea hilo, shinikizo sasa likitolewa kwa serikali kukomesha visa hivyo.

Askofu wa kanisa la Katholiki mjini Mombasa Martin Kivuva ni wa hivi punde kujitokeza kukemea vikali visa vya utekaji nyara pamoja na mauaji ya kiholelea ambayo yamekuwa yakishuhudiwa humu nchini.

Akizungumza na wanahabari katika Kanisa la Holy Ghost Cathedral mjini Mombasa kabla ya Misa ya kuadhimisha Sikukuu ya Krisimasi mnamo Jumatano Askofu Kivuva alisema visa hivyo vinaharibu sifa za taifa la Kenya na kulirejesha taifa katika nyakati mbovu za utawala wa kikoloni.

Kivuva akiitaka serikali kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote wanaoendeleza dhulma hizo za utekaji nyara, akisema kuwa iwapo vijana wana hatia wanapaswa kukamatwa na si kutekwa nyara.

Watu kushikwa kwa sababu ya msimamo Fulani au kujieleza kwa uwazi, haya ni mambo yalipitwa na wakati mambio ya Ukoloni, Tunamsihi Rais kama anajua wanaohusika hili linaturejesha nyuma zama za ukoloni haya haya mambo hatajenga imani ya vijana wetu wa kesho.” Alisema.

Kufikia sasa, Bernard Kavuli, Peter Muteti na Billy Mwangi wameripotiwa kutoweka na kanda za video zikionesha wakichukuliwa kwa nguvu zilionekana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Vijana hao walitoweka baada ya kutoa machapisho yenye utata kwenye mitandao ya kijamii.

Utekaji nyara huo umezua taharuki kote nchini Kenya, ambapo polisi wanalaumiwa kwa kuwachukua kwa nguvu watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Askofu huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Katholiki nchini ameshinikiza uwajibikaji katika vita dhidi ya ufisadi akisema ufisadi unahujumu maendeleo muhimu humu nchini, huku akiitaka serikali kukubali kukosolewa inapofanya maamuzi yasiyo sawa kwani hiyo ndio nguzo msingi ya uongozi bora.

ufisadi umekuwa kama wimbo tunaimba halafu tukienda kulala tunasahau. Tunapaswa kuondoa mambo ya ufisadi na kujenga nchi ambayo tuna viongozi waadilifu wanaojali kuhusu nchi yetu na watu wake, sio kuiba kila kitu kwa maslahi yao binafsi katika ngazi zote.” akasema.

Kuhusu ujumbe wake wa Krismasi Kiongozi huyo wa Kanisa Katholiki Mjini Mombasa aliwarai wakenya kudumisha amani na umoja katika kipindi hiki cha sherehe huku akiwataka waliombee taifa la Kenya ili lizidi kupiga hatua kimaendeleo licha ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi.

By Mjomba Rashid