Serikali imesitisha kwa muda oparesheni ya kiusalama inayoendelea katika eneo la Kapedo katika kaunti za Turukana na Baringo ili kutoa nafasi kwa viongozi kutafuta mwafaka.
Mshirikishi wa utawala katika eneo la bonde la ufa George Natembea amewapa viongozi hao siku thelathini kuhakikisha Amani inarejea katika maeneo yanayokumbwa na utovu wa usalama.
Akizungumza na viongozi hao baada ya kukamilika kwa mkutano wa kujadili njia za kuleta Amani, Natembea amesema kwamba iwapo watashindwa basi oparesheni hio itaendelea.
Haya yanajiri huku viongozi wa kaunti za Baringo na Pokot magharibi wakitoa wito kwa serikali kuhakikisha watoto wote wanaenda shule ili kukabili utovu wa usalama katika eneo la North Rift.
Viongozi hao wakiwemo wa kisiasa, wa kidini na hata wataalamu kwenye kaunti hizo mbili wanasema serikali inafaa kuhakikisha watoto wanaendelea na masomo.
Wakiongozwa na seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio, wamesema tatizo la ukosefu wa usalama linasababishwa na tamaduni zilizopitwa na wakati haswa wizi wa mifugo kauli iliyosisitizwa na seneta wa Baringo Gideon Moi.