Seneta wa kaunti ya Bungoma Moses Wetangula anaendelea kupinga hatua ya serikali ya Kenya kulipatia shirika la kimataifa la kushughulika wakimbizi UNHCR makataa ya wiki mbili kutoa mpango wa kuzifunga kambi za wakimbizi za Kakuma na Dadaab.
Wetangula anasema wiki mbili pekee hazitoshi kwa mataifa ambayo wannachi wake wanaishi katika kambi hizo, kujiandaa kuwapokea.
Wetengula ambaye aliwahi kuwa waziri wa masuala ya nchi za kigeni, amesema kuna kanuni za kimataifa za kuwashughulikia wakimbizi na ni sharti Kenya iheshimu kanuni hizo.
Kulingana na Wetangula Kanuni hizo zinatoa mwelekeo kwamba Kenya ina jukumu la kuhakikisha wakimbizi hao wanapata makao mbadala kabla ya kuzifunga kambi hizo.
Kuhusu mvutano unaoendelea baina ya Kenya na SOMALIA kuhusu mpaka wenye utajiri wa mafuta na gesi akisema haufai kutumika kuwahangaisha wakimbizi hao.
Kulingana na takwimu za UNHCR Dadaab ina zaidi ya wakimbizi laki mbili na Kakuma ina zaidi ya wakimbizi laki moja na elfu 90.