Kamati inayoshughulikia janga la Corona katika kaunti ya Mombasa pamoja na baadhi ya wanasiasa wanatazamiwa kuzuru kivuko cha Likoni Ferry pamoja na daraja la kuelea lililoko eneo la Liwatoni juma lijalo ili kutathmini hali katika sehemu hizo mbili.
Hatua hii inajiri baada ya kamati hio inayoongozwa na gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho pamoja na kamishna wa kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo kutoa agizo la watumizi wa kivuko cha Likoni kulazimishwa kutumia daraja la kuelea nyakati za asubuhi na jioni hatua ambayo inanuia kuthibiti msambao wa virusi vya corona katika kaunti ya Mombasa.
Hata hivyo, agizo hilo lilipokelewa na hisia kinzani huku baadhi ya viongozi wa Mombasa akiwemo seneta pamoja na wabunge wakipinga agizo hilo.
Kwa muda wa mwezi mmoja sasa watumizi wa kivuko hicho wamekuwa wakilazimika kutumia daraja hilo tangu mwezi machi tarehe 31 hatua ambayo watumizi hao wameikosoa pakubwa kutokana na msongamano mkubwa unaoshuhudiwa.
Na Nick Waita