Viongozi wa kaunti ya Tana River wamependekeza kuondolewa kwenye gazeti rasmi la serikali ekari 2000 za shamba la mradi wa kunyunyiza maji NIB wa Hola kaunti hiyo.
Wakiongozwa na mbunge wa Galole, Said Hiribae marufu Said Posta, viongozi hao wametaka sehemu ya mradi huo kuondolewa kwenye gazeti la serikali na kugawiwa wanainchi kama njia ya upanuzi wa mji wa Hola unaozingirwa na shamba hilo la NIB.
Mapendekezo hayo yaliyoungwa mkono na wakaazi wa eneo hilo ambao wamesema kuwa ni sharti shamba hilo ligawanywe sawia na wao kupatiwa hati miliki.
Aidha Wakaazi hao wamewakashifu wale wanaopinga mapendekezo hayo wakisema kuwa hawana nia ya kuwatoa wakaazi katika uskwota ambao umekithiri katika eneo hilo.
Hatahivyo wakaazi katika eneo hilo wameonywa dhidi ya kujenga katika shamba hilo kwa sasa wakielezwa kuwa makazi wanayoyajenga yatavunjwa hivyo wasitishe ujenzi huo hadi pale watakapopata mwafaka kamili wa swala hilo.