Mkanganyiko umeibuka kuhusu kuendelea kutelezwa kwa masharti mengine ya kukabiliana na maradhi ya Corona kufuatia hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuondolewa kwa amri ya kutotoka nje nyakati za usiku maarufu curfew.
Katika mtandao wa Twitter, Tume ya Huduma za Polisi NPSC imeweka wazi kwamba agizo la Rais la kuondolewa kwa marufuku hayo, kamwe haliathiri kutekelezwa kwa masharti mengine likiwemo la kufungwa kwa Baa na mikahawa pamoja na maeneo mengine ya burudani kuanzia saa moja usiku na hivyo kuwaonya wamiliki kwamba atakayepatikana akikiuka amri hiyo atakabiliwa kwa mujibu wa sheria.
Wakati uo huo Waziri wa Utalii Najib Balala amezitaka Baa na Mikahawa pamoja na maeneo ya Burudani kuhudumu nyakati za usiku akisema kwamba agizo la Rais la kuondolewa kwa marufuku ya kuwa nje nyakati za usiku, limeipa fursa sekta ya Utalii kunawiri tena baada ya kipindi kirefu cha Corona.
Itakumbukwa kwamba katika maadhimisho ya Mashujaa, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuondolewa kwa marufuku hayo akisema kwamba ni wakati sasa wa uchumi kufunguliwa akiwahimiza wananchi kuendelea kuchanjwa vile vile kufuata maagizo ya Wizara ya Afya.
BY NEWS DESK