HabariNews

Mpango wa Rais Uhuru Kenyatta wa kupunguza gharama ya umeme huenda ukapata pigo.

Mpango wa Rais Uhuru Kenyatta wa kupunguza gharama ya umeme humu Nchini kwa asilimia 30 kufikia Mwezi Aprili mwaka ujao huenda ukapata pigo kufuatia ufichuzi wa wizi wa fedha katika mradi wa kawi ya upepo yaani Lake Turkana Wind Power.
Kukithiri kwa ufisadi katika Wizara ya Kawi na Kampuni ya usambazaji umeme Kenya Power kunatarajiwa kuathiri mipango ya kupunguza gharama ya umeme kutokana na madeni mengi ambayo yametokana na njama za baadhi ya Wakuu Serikalini.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Kenya Power ilifaa kulipa shilingi bilioni 18 za kusambaza umeme katika eneo la Noiyengalani hadi katika kituo cha suswa.
Hata hivyo, mpango huo umekwama kutokana na Wizara ya Kawi kushindwa kulipia shilingi bilioni 9, licha ya Kenya Power kulipia shilingi bilioni 10 awali hivyo kuwa mzigo kwa Wakenya watakaolipia huduma za umeme ambazo hazikutolewa.
Katika mahojiano na Kamati ya uwekezaji wa umma katika Bunge la Kitaifa, Katibu Mkuu katika Wizara ya Kawi Gordon Kihalangwa, amebainisha kwamba sakati hiyo imetokana na hatua ya baadhi ya wakuu katika Wizara hiyo kubadili kandarasi iliyonuia Mradi wa Lake Turkana Wind Power kusambaza umeme na badala yake kuamua Kenya Power kuchukua jukumu hilo.
Haya yanajiri siku mbili tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutumia maadhimisho ya Jamuhuri kutoa ahadi ambayo, inafaa kuanza kutekelezwa rasmi Mwezi huu.

BY NEWSDESK