HabariNews

Huenda uhaba wa kawi nchini ukatatuliwa na serikali ya Kenya.

Huenda uhaba wa kawi nchini ukatatuliwa na serikali ya Kenya kufuatia lengo la kuanzisha mradi wa kisasa wa uzalishaji umeme kwa kutumia teknolojia ya nuklia kupitia ruwaza ya mwaka wa 2030.

Mkurugenzi wa maswala ya kisheria katika shirika la kawi ya nuklia (NuPEA) Justus Wabuyabo amesema kwamba mradi huo unalenga kutatua uhaba wa kawi nchini.

Akizungumza katika eneo la Diani kaunti ya Kwale, Wabuyabo amedokeza kuwa mradi huo unaotarajiwa kutekelezwa mwaka wa 2038 utaimarisha pakubwa biashara kutokana na bei nafuu ya kawi.

Kwa upande wake mkurugenzi wa maswala ya utetezi katika shirika hilo Basip Buyuka amesema kuwa tayari wameweka mipangilio ya kiusalama ya uzalishaji wa umeme kupitia teknolojia hiyo.

Haya yanajiri katika kikao kilichowaleta pamoja wadau mbali mbali wa kaunti hiyo kujadili na kutathmini athari za kimazingira za utekelezaji wa mradi huo nchini.

BY EDITORIAL DESK