Ukosefu wa maji safi kutokana na mabadiliko tabia ya nchi kutoka sehemu kame ndani ya kaunti ya Kwale umepelekea wasichana wengi wa shule maeneo hayo kudhulumiwa kijinsia.
Haya ni kwa mujib wa wazazi kutoka sehemu hizo wakiongozwa na Mwanasiti Chiliko amedokeza kwamba kiangazi kikali kinacho kumba eneo hilo kimesababisha mabwawa mengi kukauka hali inayowalazimu kutembea mwendo mrefu kutafuta maji hayo jambo alilolitaja kuchangia kunyanyaswa kimapenzi na baadhi ya wavulana wanaowasaidia kuchota na hata kuwabebea maji kufuatia umbali wa chemichemi hizo za maji.
Mama huyo amesema kwamba mabwawa machache yalio na maji kidogo yana kina kirefu na kusabisha wasichana kutoweza kuingia kuchota maji hivyo kutegemea usaidizi kutoka kwa wavulana hao ambao baadaye hudai kulipwa kwa njia ya kushiriki nao kimapenzi.
Hata hivyo kinamama hao wameitaka serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuja na mbinu mbadala za kuweza kupunguza athari za ukosefu wa maji ya kutosha na safi kwa kuwaletea mabomba ya maji safi na kuwachimbia mabwawa kila kijiji ili kupunguza unyanyasaji huo miongoni mwa wasichana hao.
BY EDITORIAL TEAM