HabariNews

Viongozi wa kidini kutoka kaunti ya Kwale wamezindua mpango wa kukabiliana na tatizo la utumizi wa mihadarati miongoni mwa vijana.

Viongozi wa kidini kutoka kaunti ya Kwale wamezindua mpango wa kukabiliana na tatizo la utumizi wa mihadarati miongoni mwa vijana.

Mpango huo unatarajiwa kutekelezwa na viongozi 200 wa dini ya kiislamu na kikristo katika maeneo ya Msambweni na Lungalunga kupitia mradi wa Faith Community Against Drugs and Substance Abuse (FACADA).

Wakiongozwa na Askofu wa kanisa la FPFK David Kiragu na katibu wa baraza la kitaifa la ushauri kwa waislamu nchini (KEMNAC) Sheikh Amani Hamisi, viongozi hao wameahidi kupambana na utumizi wa dawa za kulevya katika maeneo hayo.

Mradi huo wa majaribio unatarajiwa kutekelezwa kwa muda wa mwaka mmoja kupitia ufadhili wa serikali ya Denmark.

Afisa msimamizi wa mradi huo Emmanuel Kahso amesema kuwa viongozi hao wanatarajiwa kuhubiri katika sehemu za ibada kuhusu athari za utumizi wa dawa hizo miongoni mwa vijana.

Kwa upande mwingine ipo haja ya serikali ya kaunti ya Kwale kuwahamasisha na kutoa ushauri nasaha kwa vijana wanaotumia dawa za kulevya dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Haya ni kwa mujib wa mkurugenzi wa shirika la kijamii la watumizi wa midarati kaunti ya Kwale KWANPUD,Ahmed Said amesema kuwa waraibu wanaojidunga sindano wapo katika hatari kubwa ya kuambukizana zaidi na hata wapendwa wao walio nao kwenye ndoa iwapo juhudi zaidi hazitoelekezwa kwao.

Said ameendelea kusema asilimia 18.7 ya waraibu hao wapo katika hatari hiyo jambo alilolitaja kutia hofu miongoni mwao.

Wakati uo huo mkurugenzi huyo ameitaka serikali ya ugatuzi kuboresha huduma zao kwa waraibu hao ikizingatiwa kwamba idadi ya waraibu wanaopewa tiba ya methadone inazidi kuongezeka kila uchao.

Aidha Said amesema kutokana na idadi ya waraibu kuongezeka wanashinikiza uongozi wa kaunti hiyo kukamilisha ,kutuma wahudumu watakao washughulikia waraibu katika kituo cha afya cha Ganja la Simba na kupanuliwa kwa kituo cha kombani ili kupunguza msongamano wanapofuata huduma za kiafya.

BY EDITORIAL TEAM