Spika wa bunge la kaunti ya Kwale Seth Mwatela amesema kuwa watahakikisha miswaada inayohusiana na watu wenye ulemavu inaangaziwa pakubwa ili kuwapa watu wenye mahitaji maalum nafasi sawa na wengine.
Akizungumza katika eneo la Msambweni kaunti ya Kwale Mwatela amesema kuwa bunge la kaunti tayari linashughulikia miswaada inayohusu walemavu huku akisema katika maswala ya zabuni watu hao watapewa kipaumbele.
Haya yanajiri baada ya jamii ya watu wenye mahitaji maalum kulalamika kuhusiana na kutengwa huku vyama vya kisiasa katika kaunti ya Kwale vikikosa kuteua walemavu katika bunge hilo.
Mwalimu Ali ni mmoja wa watu wenye mahitaji maalum na ameitaka kaunti kuja na mbinu maalum ya kukusanya takwimu kujua idadi ya walemavu kando na kubuni kamati maalum katika kaunti hiyo.
Hata hivyo, kukosekana kwa mbinu maalum ya watu wenye ulemavu kumepelekea kutokuwa na takwimu kamilifu ya watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti ya Kwale.
Haya ni kulingana na mwakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti ya Kwale Mwalimu Ali, na kwamba ukosefu wa mbinu maalum wa kuwatambua wenye mahitaji maalum hupelekea hata wao kukosa nafasi za uwakilishi.
BY EDITORIAL DESK