HabariNews

WATU 13 WAUAWA UKANDA WA PWANI KWA TUHUMA ZA UCHAWI.

Mauaji ya wazee ukanda wa Pwani yanaonekana kuongezeka kila uchao licha ya serikali kuu, mashirika ya kijamii, viongozi wa kidini na wa kisiasa kutoa hamasa za mara kwa mara.

Kulingana na takwimu kutoka shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Yetu, kaunti ya Kwale inaongoza kwa mauaji hayo ikifuatiwa kwa karibu na kaunti ya Kilifi.

Kati ya mwezi Januari hadi Machi mwaka huu, watu 7 wameuawa katika wadi Dzombo eneo bunge la LungaLunga kaunti ya Kwale huku 6 wakiuawa katika wadi ya Mariakani eneo bunge la Kaloleni, kaunti ya Kilifi.

Baadhi ya wakaazi wa Dzombo wameelezea sababu zinazochangia kutekelezwa kwa mauaji haya ikiwa ni rasilimali, mipaka kwenye mashamba, mizozo ya kijamii, miongoni mwa sababu zingine lakini kuu Zaidi ikiwa ni tuhuma za uchawi.

Ikumbukwe kwamba mwezi uliopita waziri wa masuala ya ndani ya nchi prof. Kithure Kindiki alitoa wito kwa jamii za ukanda wa Pwani kusitisha mauaji ya wazee huku akisema kuwa kama wizara watahakikisha wanawasaka wale wote wanawaotishia wazee maisha.

BY JOYCE KELLY