Kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga ameahidi kutangaza hivi karibuni mpango wa kugomea baadhi ya bidhaa na kampuni anazodai kuhusika na serikali.
Akihutubia wafuasi wake katika kaunti ya Migori Raila amezilaumu baadhi ya kampuni na hata vyombo vya habari anavyodai vimekuwa vikitumiwa vibaya na serikali tawala.
Odinga amesema wiki ijayo makao makuu ya Azimio yatatoa taarifa na maelekezo kwa wakenya kuhusu bidhaa na kampuni ambazo watazisusia.
“Kuna bidhaa kadhaa makao yetu makuu itatoa taarifa tuwaambie bidhaa hizo muachane nazo, kampuni hizo muachane nazo. Kuna kampuni kadhaa ambazo tunajua zinatumiwa vibaya na hawa watu. Wiki ijayo tutawaambia nyinyi hizi kampuni muwache, hii gazeti msinunue, hii radio msisikize, sawa sawa.” Akasema Odinga.
Wakati uo huo Raila ametetea hatua ya muungano wake kushinikiza mchakato wa maandamano nchini akisema kuwa wananchi hawakuwa na budi kutumia hatua hiyo kwani ni haki yao ya kikatiba.
Raila amesiistiza kuwa njia pekee ya kuwasilisha malalamiko kwa serikali ni kupitia maaandamano huku akidai baaadhi ya viongozi wamekosa kutekeleza wajibu wao wa kuwasilisha malalamiko ya wananchi kwa serikali na badala yake kushawishiwa kupitia hongo.
Huku hayo yakijiri Muungano wa Azimio la Umoja umeteua jopo la watu watano litakalowawakilisha katika mazungumzo ya maridhiano yanayotarajiwa kuendeshwa baina yao na viongozi wa Kenya Kwanza.
Watano hao wataongozwa na Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa wachache katika bunge Opiyo Wandayi na kiongozi wa chama cha DAP Eugene Wamalwa huku Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni na Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi wakikamilisha kikosi hicho.
BY EDITORIAL DESK